WAWILI WAUAWA KIKATILI SHINYANGA,MMOJA ANYONGWA KWENYE MTI,MWINGINE ATUPWA CHINI YA DARAJA

 
Mwanamme asiyefahamika jina wala makazi yake ameuawa kwa kunyongwa shingo kisha mwili wake kutundikwa juu ya mti kwa kutumia suruali aliyokuwa amevaa na watu wasiofahamika katika kijiji na kata ya Ibadakuli manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga.


Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SSP Longinus Tibishubwamu alisema tukio hilo limetokea Januari 27,mwaka huu saa 10:46 jioni katika kijiji cha Ibadakuli ambapo mwanamme (30-35) huyo asiyejulikana jina,kabila wala makazi yake aliuawa kisha mwili wake kutundikwa juu ya mti.


Kamanda Tibishubwamu  alisema mwanamme huyo aliuawa na watu wasiofahamika kisha mwili wake kutundikwa juu ya mti kwa kutumia suruali aliyokuwa amevaa.


Alisema mwili wa marehemu umekutwa na jeraha kwenye kidole cha mguu wa kulia na uchunguzi wa daktari unaonyesha kuwa marehemu alinyongwa shingo na chanzo cha mauaji hayo bado hakijajulikana.


Wakati huo huo mwanamke asiyefahamika jina wala makazi yake anayekadiriwa kuwa na umri kati ya 25 na 30 ameuawa kisha mwili wake kuwekwa chini ya daraja dogo lililopo katika kitongoji cha Jihingu kata ya Kolandoto manispaa ya Shinyanga.


Kamanda Tibishubwamu  alisema tukio hilo limetokea Januari 27,mwaka huu saa 12:00 jioni katika kitongoji cha Jihingu ambapo mwanamke huyo aliuawa na watu wasiofahamika kisha mwili wake kuwekwa chini ya daraja dogo lililopo katika kitongoji hicho.


Aliongeza kuwa mwili wa marehemu umekutwa ukiwa na majeraha kichwani,usoni na ubavu wa kulia na kwamba jeshi la polisi linafanya uchunguzi juu ya mauaji hayo ili kuwabaini na kuwakamata wahusika.

Na Kadama Malunde-Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527