![]() |
| Wanahabari wakijiandaa kupanda ndege kutoka Dar es salaam kuelekea Accra via Nairobi |
Na mwandishi wa Malunde1 blog-Accra Ghana
Ziara
ya Mafunzo ya waandishi na viongozi wa vyombo tisa vya habari kutoka Tanzania
nchini Ghana, imekuwa ya mafanikio makubwa kufuatia timu hiyo kujionea mambo
mbalimbali ya muhimu katika uboreshaji wa sekta ya habari nchini Tanzania.
Meneja
wa Radio Kahama FM Marco Mipawa amevifahamisha vyombo vya habari nchini kwamba,
yeye pamoja na washiriki wenzake 8, wamekubali kwamba kuna umuhimu wa kufanyika
mabadiliko makubwa katika sekta ya habari nchni, ili iwe kama ilivyo nchini
Ghana.
Mipawa amekiri kufurahishwa na uhuru wa vyombo
vya habari nchini Ghana, ambapo huwa vinafanya shughuli zake kwa uhuru mkubwa
katika uibuaji wa agenja za kuzuia uovu dhidi ya serikali bila vitisho
vyovyote.
Naye
Meneja wa Jogoo FM Radio ya mjini Songea Magira Magira amesema amejifunza
umuhimu wa kutazama kipaji cha mtu katika utangazaji ili jamii imkubali, na
kwamba elimu ni kitu cha ziada katika kusaidia kukilinda na kukiboresha kipaji
hicho.
Kwa
upande wake Meneja Masoko na Mhasibu wa Kahama FM Radio ya mjini Kahama Letcia
Kagoro amesema, alichojifunza ni umuhimu wa kuwekeza katika raslimali watu na
vitu, kabla ya kuanza uendeshaji wa mradi wowote ikiwemo miradi ya Redio.
Amekiri
kwamba, mafanikio yanaweza kufikiwa kwa kuweka malengo ya muda mfupi na mrefu
yanayopimika katika uendeshaji wa redio, tv na vyombo vingine; ili kuwa na
mwongozo katika utekelezaji wa kazi na tathmini yake.
Wakati huo huo,
mkuu wa msafara huo na mmiliki wa Radio CG FM kutoka Tabora Charles George, amewaasa wamiliki na waajiri wa Redio kutambua
vipaji vya watumishi wao kabla ya kuwaajiri, kuviendeleza na kuvilinda kwa
gharama yoyote.
Naye
mwandishi kutoka Triple A FM ya mjini Arusha Marick Munga amesema,
alichojifunza ni umuhimu wa vyombo vya habari kufanya tafiti za kina kwa jamii
ili kubaini mahitaji yake kabla ya kuibua agenda zinazoihusu.
Meneja
wa Standard Radio iliyoko mjini Singida Alice Achieng amefurahishwa na tabia ya ushirikiano wa wafanyakazi katika vipindi
mbalimbali redioni na televisheni,ambapo kwa kila kipindi daima huwa pamoja ili
kuhakikisha wamepeleka ujumbe ambao jamiia inauhitaji
Timu
hiyo ya wanahabari kutoka Tanzania nchini Ghana, jana imemaliza program ya
kutembelea kituo cha Multimedia Group LTD kilichoko jijini Accra, ambapo wiki
ijayo itatembelea vituo vingine vya habari mjini Kumasi nchini humo.
Wanahabari hao kutoka Tanzania wameahidi kuja kuhamasisha mabadiliko katika uendeshaji wa vipindi vya redio nchini, ili vilenge watu na maisha yao kwa nia ya kufichua uovu na kuwaletea maendeleo.
Ziara ya viongozi tisa wa vyombo vya habari kutoka Tanzania nchini Ghana, ilianza Desemba mosi mwaka huu na wanatarajia kurudi nchini Desemba 15 mwaka huu ambapo mafunzo hayo ya wiki mbili yamefadhiliwa na mfuko wa kusaidia vyombo vya habari nchini TMF.

Social Plugin