POLISI WALIIBEBA CCM HUKO CHALINZE

Waangalizi katika Uchaguzi wa Ubunge Chalinze wamesema Jeshi la Polisi lilielekeza ulinzi kwenye mikutano ya CCM zaidi na kuviacha vyama vingine vikiwa havina ulinzi. 

Waangalizi hao ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Mashirika ya Haki za Binadamu Kusini mwa Afrika (Sahringon) walisema vyama vya Chadema, CUF, NRA na AFP havikupewa na ulinzi.
Akizungumza jana, Mratibu wa Taifa wa Sahringon, Martina Kabisama alisema ulinzi wa polisi ulikuwa kwenye mikutano ya CCM na si kwa vyama vingine hali ambayo ingeweza kuathiri usalama wa maeneo hayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei hakupatikana jana kuzungumzia madai hayo, lakini msaidizi wake, Steven Kiango alisema bosi wake atalitolea ufafanuzi suala hilo, Jumatatu. “Kwa sasa Kamanda Matei yuko nje ya ofisi na siwezi kulizungumzia hilo, nitamfahamisha na atalitolea ufafanuzi Jumatatu,” alisema Kiango.
Kabisama alisema: “Kwa mfano, siku ya kufunga kampeni timu ya uangalizi ilishuhudia ulinzi mkubwa kwenye mikutano ya CCM lakini Chadema na CUF hakukuwa na askari hata mmoja,” alisema.
Alisema waangalizi hao pia walibaini lugha za maudhi, kashfa na kejeli katika kampeni za vyama vya CCM, Chadema na CUF.

 “Tunapendekeza Msajili wa Vyama vya Siasa atoe karipio kali kwa vyama hivyo kuhusu matumizi ya lugha za vitisho, kashfa na kejeli,” alisema.
Alipendekeza kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kuifanyia marekebisho Sheria ya Uchaguzi ili kuwazuia viongozi wakuu wa serikali  kushiriki kwenye kampeni.
 Na Raymond Kaminyoge na Sanjito Msafiri

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post