BRN Hoi Kishapu!!!! WALIMU WAISHI KWENYE MADARASA,TAZAMA PICHA HAPA,NI SHIDAAAAA!!!

Ni katika shule ya msingi Mwamashimba kata ya Mwamalasa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga,hapa ni ndani  ya moja ya madarasa katika shule hiyo kongwe iliyoanzishwa mwaka 1976 kama unavyoona hapo sakafuni ni kokoto mwanzo mwisho.


 Jengo la darasa katika shule ya msingi Mwamashimba linalotumika kama makazi ya walimu.
Jengo  la mwanzo kabisa katika shule ya msingi Mwamashimba ambalo hivi sasa linatumika kama jiko kwa ajili kupikia uji kwa wanafunzi,shule hiyo ni miongoni mwa shule ambazo zinapata huduma ya uji katika wilaya ya Kishapu
Choo katika shule ya msingi Mwamashimba ambacho kimekwama ujenzi wake.Hapo ni upande wa mbele wa choo hicho,katika upande wa nyuma katika choo  hicho baadhi ya matundu yanatumiwa na wanafunzi wa shule hiyo kutokana na ukosefu wa choo katika shule hiyo. 
Moja ya matundu ya vyoo katika choo ambacho hakijakamilika  ujenzi wake kinachotumiwa na wanafunzi wa shule ya msingi Mwamashimba kutokana na ukosefu wa choo katika shule hiyo.
Shule ya msingi Mwamashimba iliyopo katika kijiji cha Mwamashimba kata ya Mwamalasa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa choo,uhaba wa madawati na nyumba za walimu ambapo hivi sasa walimu wanalazimika kuishi kwenye vyumba vya madarasa.

Hayo yamebainika juzi baada ya waandishi wa habari kutembelea shule hiyo na kujionea hali halisi ya mazingira ambapo walishuhudia walimu wakitumia vyumba vya madarasa kama makazi yao katika shule hiyo.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Elias Zengo alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1976 ina jumla ya wanafunzi 492 na walimu tisa pekee wa kiume 8 na mwalimu wa kike mmoja.

Alisema tatizo kubwa linaloikabili shule hiyo ni upungufu wa nyumba za walimu kwani zilizopo sasa ni nyumba mbili pekee hali inayowafanya baadhi ya walimu kuishi kwenye vyumba vya madarasa.

Mwalimu Zengo inakabiliwa na ukosefu wa choo cha wanafunzi hali inayowafanya wanafunzi kutumia choo ambacho hakijakamilika baada ya ujenzi wake kukwama na kuongeza kuwa pia upungufu wa madawati unasababisha baadhi ya wanafunzi kukaa chini.

“Kuna baadhi ya wanafunzi wanalazimika kukaa chini,hii ni changamoto na madarasa haya hayajasakafiwa,madarasa mengine yana kokoto,hata hivyo tayari kuna fedha zimetengwa na halmashauri ya wilaya kwa ajili ukarabati wa madarasa haya”,aliongeza mwalimu Zengo.

Kwa upande wake afisa mtendaji wa kijiji cha Mwamashimba ilipo shule hiyo Julius Emmanuel alikiri kuwepo kwa changamoto hizo na kuongeza kuwa wanajiandaa kufanya mkutano na wananchi ili kuangalia namna ya kuzitatua hizo kama vile kuchanga pesa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu.

“Mara nyingi,wananchi wa kijiji hiki wamekuwa mstari wa mbele kuchangia miradi ya maendeleo,hata ujenzi wa choo ambacho hakijakamilika umetokana na nguvu zao,na ujenzi ukifikia usawa wa renta ndiyo huwa tunaomba msaada kutoka serikalini”,alisema afisa Mtendaji.

Naye diwani wa kata ya Mwamalasa ilipo shule hiyo ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu Justine Sheka alisema suala la walimu kuishi kwenye vyumba vya madarasa linatokana na shule hiyo kutokuwa na wanafunzi wa kutosha na kutokana na upungufu wa nyumba za walimu.

“Shule hii ni kongwe imejengwa mwaka 1976,mimi ni diwani wa kata hii kupitia CCM tangu mwaka  1994, shule hii ilikuwa na madarasa ya tope ,tukajenga mapya ,wanafunzi wakawa wachache,na kwa sababu ya upungufu wa nyumba za walimu tukatumia busara kuyageuza  baadhi ya madarasa kuwa nyumba za walimu”,alisema Sheka.

Hata hivyo Sheka alisema tayari jumla ya shilingi  milioni 9 zimetengwa  na halmashauri ya wilaya ya Kishapu kwa ajili ya ujenzi wa vyoo katika shule hiyo na shilingi milioni 30 kwa ajili ya madawati katika shule za msingi wilayani humo ikiwemo shule ya msingi Mwamashimba.


Na Kadama Malunde-Kishapu

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post