Duh!! Hii sasa Balaa !! MWALIMU MKUU SHULE YA MSINGI AFUNGUA BAA SHULENI

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, shule ya Msingi Unenamwa kata ya Luwumbu wilayani Makete mkoa wa Njombe imeingia kwenye hali ya sintofahamu baada ya mwalimu mkuu wa shule hiyo kudaiwa kufungua baa shuleni hapo


Tukio Hilo la aina yake limeonekana kuwachefua wananchi Kwa kuwa si kawaida kutokea kitendo kama hicho kufuatana ma maadili ya taaluma ya ualimu

Akizungumzia suala hilo mwenyekiti wa serikali ya Kijiji cha Unenamwa Bw. Labson Tweve amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kusema biashara hiyo ya baa shuleni hapo imedumu kwa zaidi ya mwaka mmoja

“Ndugu mwandishi wa habari ni kweli kabisa mwalimu huyo amekuwa akiuza pombe kwenye nyumba yake (nyumba ya mwalimu iliyojengwa na serikali), na anauza bia na pombe za kienyeji ikiwemo Msabe” amesema Mwenyekiti huyo

Amesema watu mbalimbali wamekuwa wakijiendea kwenye nyumba ya mwalimu huyo kwa ajili ya kununua na kunywa pombe kwa kuwa wameshazoea eneo hilo kuwa ndipo wanapojipatia huduma

Naye mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Bw. Nyaluke Haruni amesema walishawahi kumwita mwalimu huyo kwenye vikao vya kamati yake na kumuonya pamoja na kumzuia kuuza pombe kwenye nyumba hiyo ambapo aliacha kuuza hadharani na badala yake akaamua kuuza kwa siri

“Ukienda kama mtafiti si rahisi kugundua lakini mteja akienda kwenye nyumba hiyo anapatiwa huduma anayoitaka (huduma ya pombe) halafu anaondoka” alisema

Wakizungumza kwa masharti ya kuhifadhiwa majina yao, baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi wetu wamesema wananchi wamekuwa wakijiendea nyumbani kwa mwalimu mkuu huyo kununua pombe na suala hilo limekuwa likiendelea kukua siku hadi siku
“Ni kweli idadi ya watu wanaokwenda kwenye nyumba ya mwalimu huyo kununua na kunywa pombe ni kubwa ingawa wapo wanaokwenda kwa kujificha na wengine wanakwenda bila woga” walisema wananchi hao wanaoizunguka shule hiyo

Akizungumzia tuhuma hizo mwalimu mkuu wa shule hiyo Mwl. Evalisto Johanes amekanusha vikali tuhuma hizo zinazoelekezwa kwake na kusema yeye hajawahi na hafanyi biashara hiyo ya kuuza pombe nyumbani kwake

Mwl. Johanes amesema yeye kama mwalimu mkuu anatambua maadili ya kazi yake kuwa hayaruhusu kuuza pombe shuleni, na yeye anauza vitu vidogo vidogo kwa wateja wake ambavyo si pombe

“Hilo jambo si la kweli ndugu mwandishi, mimi siuzi bia wala pombe za kienyeji na badala yake natoa mahitaji madogo madogo, kama soda na hizi ni kwa ajili ya wageni wangu wanaonitembelea hapa nyumbani” alisema mwalimu mkuu huyo

Amesema watu wasizungumze maneneo ambayo hawana uhakika nayo, na kuongeza kuwa nyumbani kwake hakuna huduma yeyote ya kilevi inayotolewa na yeye

Afisa elimu shule za msingi wilaya ya Makete Bw. Antony Mpiluka akitolea ufafanuzi sakata hilo amesema kiutaratibu hairuhusiwi mwalimu kuuza pombe kwenye eneo la shule na endapo atafanya hivyo anatakiwa kuchukuliwa hatua kwa kufuata ngazi husika kuanzia chini hadi juu

Bw. Mpiluka amesema anashangazwa na serikali ya kijiji ambao ndio wamiliki wa shule hiyo kulifumbia macho suala hilo kwa zaidi ya mwaka mmoja, na mwenyekiti wa kijiji ambaye ndiye mwenye mamlaka ameshindwa kulitolea maamuzi suala hilo na badala yake anakuwa mlalamikaji

“Shule hiyo ipo chini ya serikali ya kijiji, kama mwalimu huyo anauza pombe shuleni wao ndio walitakiwa wawe wa kwanza kumuita na kumhoji na baadaye wachukue hatua, wakishindwa waandike barua wilayani kwa ajili ya hatua zaidi na si wao kama serikali ya kijiji ambayo inamamlaka zote inageuka kulalamika badala ya kutenda, wao ni watendaji na si walalamikaji” alisema Mpiluka
via>>Eddy blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments