CCM WADAIWA KUMPA KICHAPO KIONGOZI WA KANISA LA ORTHODOX HUKO KALENGA IRINGA

 Paroko wa Kanisa la Orthodox, Parokia za Nyamihuu Kalenga, Iringa, Costantino Mbilinyi akizungunza na waandishi wa habari nyumbani kwake katika Kijiji cha Nyamihuu jana kuhusu kushambuliwa kwake Kalenga. 
 
Padri wa Makanisa ya Orthodox katika Kijiji cha Nyamihuu, Kata ya Nzihi, jimboni Kalenga Constantino Mbilinyi (36) amepigwa na kujeruhiwa na watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa CCM.
 
 Baada ya kukutwa na mkasa huo, Padri Mbilinyi alishikiliwa kwa muda katika Ofisi ya Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Kumbusho Chengula, na baadaye alichukuliwa na askari ambao walimpeleka Kituo cha Polisi Kati, mjini Iringa kwa mahojiano.
 
 Kasisi huyo akizungumza na waandishi wa habari jana alisema alipatwa na mkasa huo alipoambatana na viongozi wa Chadema waliopiga kambi kwenye Kata ya Nzihi, ambao walikuwa wakielekea kwenye mikutano ya kampeni za kumnadi mgombea ubunge kupitia chama hicho, Grace Tendega.

Alisema viongozi hao walimwomba awasindikize kwenda Kijiji cha Igangimali kwa ajili ya kumwona mtu aitwaye, Samti Ngonjela ili wamkabidhi mabango Tendega. 
 
“Waliniomba na mimi nikakubali kwa kuwa nilikuwa na ratiba ya kwenda katika kijiji kile kumwona Bento Ngaila ambaye tulitaka kuzungumza kuhusiana na mchakato wa shamba langu lililoko katika kijiji kile,” alisema Mbilinyi na kuongeza:
 
 “Tulipofika nilimtafuta Ngonjela kwa ajili ya kuwaonyesha viongozi wa Chadema, lakini wakati huo vijana wengine wa Chadema walianza kubandika mabango ya mgombea katika klabu ya pombe ya Lazaro Nzigi, na ghafla lilitokea kundi la wanachama wa CCM na kuanza kuwafukuza.”

Alisema vijana hao walimgeukia wakimshutumu kwamba aliwapeleka watu wa Chadema katika eneo lile ambalo wao walikuwa na mkutano wa ndani. 
 
Mbilinyi alisema licha ya kujitetea, wafuasi hao wa CCM walimkamata na kumwangusha na kumfunga mikono nyuma kwa kamba ya katani.
 
 Wakati huo wafuasi wa Chadema walikuwa wameshaondoka. “Walianza kunipiga na kunisukuma hali iliyonifanya nianguke chini na kuumia mkononi na mgongoni.
 
 Nikiwa nimeanguka chini na mikono yangu imefungwa kamba kwa nyuma mmoja wa vijana hao alichukua pilipili na kuingiza kwenye mfuko wa shati langu kisha wakanichukua na kunipeleka ofisi ya ofisa mtendaji iliyoko Nyamihuu,” alisema Mbilinyi.

Mbilinyi alisema makada hao wa CCM walimweleza ofisa huyo kwamba alikwenda na wenzake kuwafanyia fujo na kwamba aliwatukana na kuwatishia maisha. Alisema watu waliomfanyia unyama huo anawafahamu.

Ofisa Mtendaji
Kaimu Ofisa Mtendaji, Chengula alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa alilazimika kumweka ndani kwa kuhofia hali ya usalama.
 “Ni kweli....nilipigiwa simu na kada wa CCM ninayemfahamu akaniambia Padri huyo amepeleka wanachama wa Chadema kwenye eneo ambalo wao walikwenda kuwatembelea wanachama wao na kwamba waliwatukana,” alisema Chengula na kuongeza:
 “Ilipofika saa 12 jioni niliona kundi la watu wakija ofisini huku wakiwa wamemtanguliza Mbilinyi ambaye alikuwa amefungwa kamba mikononi.” 
 
Alisema baada ya kupokea maelezo ya makada wa CCM aliamuru Padri Mbilinyi afanyiwe upekuzi kisha alimweka ndani lakini baadaye saa 5 usiku polisi wakiongozana na viongozi wa Chadema na CCM walifika kisha kuondoka naye.

CHADEMA, CCM
Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo ya Ufundi, Benson Kigaila alisema alikwenda polisi kumwekea dhamana. Aliwapongeza polisi kwa kufika haraka Kata ya Nyamihuu ambako ndiko alikokamatwa padri huyo na kupigwa. Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Iringa, Delfina Mtavilalo alisema: 
 
“Huyo padri ninamfahamu lakini taarifa kwamba alipigwa na wafuasi wa CCM hazina ukweli wowote.” Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mungi hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo na simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa. 
Chanzo- zeangazio blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post