Mnyukano wa CCM!! MAKADA WA CCM KIFUNGONI KWA MIEZI 12 TENA CHINI YA UANGALIZI,YUMO LOWASSA NA SUMAYE

Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imetangaza uamuzi mzito dhidi ya wanachama wake sita ambao hivi karibuni waliitwa na Kamati Ndogo ya Maadili na kuwahoji kutokana na tuhuma za kuanza kabla ya wakati kampeni za Uchaguzi Mkuu wa urais wa mwaka 2015.
CCM imewatia hatiani vigogo wote sita kwa makosa ya kujihusisha na kampeni za uchaguzi kabla ya wakati, hivyo kuwafungia kugombea nafasi za uongozi ndani ya chama hicho kwa miezi 12, pia wakiwa chini ya uangalizi.
Waliokumbwa na adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari jana alisema wanachama hao wote sita walitiwa hatiani kwa makosa ya kuanza kampeni za kuusaka urais wa 2015 kabla ya wakati jambo ambalo ni kinyume na taratibu za chama hicho, hivyo kutoa onyo kali. 
Adhabu ya onyo kali kwa mujibu wa taratibu za chama hicho inamaanisha kuwaweka chini ya uangalizi kwa miezi 12 ili kuhakikisha hawajihusishi na vitendo vyovyote vinavyokwenda kinyume na misingi ya chama hicho, vinginevyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Mwanachama aliyepewa onyo kali atakuwa katika hali ya kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi 12 ili kumsaidia katika jitihada zake za kujirekebisha,” alisema Nnauye.
Hatua hiyo ya CCM imezitia doa harakati za vigogo hao, kwani watatumikia adhabu yao hadi Februari 2015 na wakati wote watakuwa wakichunguzwa mienendo yao.
Nnauye alisema makada hao kwa kuanza kwao kampeni za kutafuta kuteuliwa kuwania urais kabla ya wakati ni kinyume na kanuni za uongozi na maadili za CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6 (7)(i).
“Wamethibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii. “Vitendo vya namna hii ni kosa kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili za CCM toleo la Februari 2010, Ibara kadhaa za kanuni hizo,” alisema Nnauye.
Alisema: “Kamati Kuu baada ya kuthibitisha makosa hayo, imewapa watu wote sita waliohojiwa adhabu ya onyo kali na kuwataka wajiepushe na vitendo vinavyokiuka maadili na iwapo wataendelea na vitendo hivyo chama kitawachukulia hatua kali.”
Alisema Kamati Kuu imeiagiza kamati ya maadili kuwachunguza mawakala na watendaji wa wanachama hao waliokuwa wakiratibu shughuli mbalimbali ili waweze kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu hatua inayolenga kuhakikisha chama hakigawanyiki.
Nnauye alisema Ibara 6 (2) (1-5) ya maadili ya viongozi wa chama hicho inawazuia kutoa michango, misaada, zawadi za aina yoyote, kukusanya michango na kufanya kampeni bila ya kupata kibali kutoka kamati ya siasa ya halmashauri ya eneo husika.
Sumaye, Membe wanena
Akizungumza jana, Sumaye alisema: “Siwezi kuzungumza chochote kwa kuwa sijapata taarifa rasmi kutoka ndani ya chama.
“Mimi sijapata taarifa yoyote, nitakapopata barua ndipo nitakaposema, kwa sasa ndiyo kwanza ninakusikia wewe ukinipa hizi taarifa,” alisema Sumaye.
Kwa upande wake, Membe naye alisema hajapa taarifa kutoka ndani ya chama na hivyo hawezi kuzungumzia taarifa za kusikia.
“Sina habari hadi sasa! Utaratibu wa Kamati ya Maadili ni kupeleka taarifa Kamati Kuu….Kamati Kuu inajadili na barua huandikwa kwa kila aliyehojiwa na kupatikana na hatia. Mimi sijapata hiyo barua na siwezi kukujibu au kutoa maoni ‘based on hearsay!’ vuta subira” alisema Membe.
Mnyukano CCM
Katika siku za karibuni kumekuwa na vita ya maneno baina ya makada wa chama hicho, wakituhumiana kwa rushwa na kutangaza mapema kugombea urais kabla ya ruhusa rasmi ya chama.
Malumbano ya sasa yalishika kasi Januari Mosi mwaka huu wakati Lowassa, alipotangaza kuanza rasmi kwa safari aliyoiita ya matumaini ya ndoto zake, ambayo alisema itatimiza ndoto za Watanzania za kupata elimu bure, maji safi na maendeleo ya uhakika.

Lowassa alitoa kauli hiyo wakati wa hafla ya mwaka mpya aliyowaandalia rafiki na jamaa zake, Januari Mosi, mwaka huu huko Monduli mkoani Arusha.

Chanzo-Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post