MKUU WA MKOA ATUHUMIWA KUTUMIA VIBAYA MADARAKA ALIYOPEWA NA RAIS

Katika kile kilicholezwa kuwa ni kutofurahishwa na hatua ya mkuu wa mkoa wa Geita, Magalula Said Magalula kuagiza kukamatwa na kuwekwa ndani kwa wawekezaji wa zao la pamba wanaofanya shughuli zao katika mkoa huo kwa madai hawajatekeleza agizo la kufunga mikataba na wakulima wa zao la pamba,Chama Cha Wakulima wa Zao la Pamba nchini (TACOGA) kimemlalamikia mkuu huyo wa mkoa  kikimtuhumu kutumia vibaya madaraka yake aliyopewa na Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania mheshimiwa Dkt Jakaya Mrisho Kikwete.


Kwa mujibu wa tamko rasmi lililotolewa kwa waandishi wa habari  mjini Kahama na mwenyekiti wa TACOGA, Elias Zizi agizo hilo linapingana na maelekezo yaliyotolewa hivi karibuni na rais Kikwete akiagiza wakulima kutolazimishwa kujiunga katika kilimo cha mkataba mpaka kwanza wapewe elimu ya kutosha.



Mwenyekiti huyo wa TACOGA alisema mapema wiki iliyopita mkuu huyo wa mkoa aliagiza kukamatwa kwa wawakilishi wa kampuni zinazonunua pamba waliokuwa wamehudhuria kikao cha wadau wa zao hilo kilichofanyika mjini Geita baada ya kuwataka watoe taarifa ya vikundi vingapi vya wakulima ambavyo wamefunga navyo mkataba.



Zizi alisema wawekezaji waliokamatwa na kuwekwa ndani kwa agizo la mkuu huyo wa mkoa kuwa ni pamoja na mwakilishi wa kampuni ya Fresho Investment, Kampuni ya ICK Cotton Co. Ltd na Kahama Oil Mill Ltd ambao wote wanafanya shughuli zao katika mkoa huo wa Geita.



Zizi alisema TACOGA wameshangazwa na hatua ya mkuu huyo wa mkoa na kudai ni matumizi mabaya ya madaraka aliyopewa na Rais Kikwete na kwamba suala la kilimo cha mkataba pamoja na kuwa ni hiari hata hivyo lilisitishwa kwa muda baada ya kujitokeza kwa changamoto kadhaa baada ya majaribio yake katika baadhi ya maeneo.



Hata hivyo mkuu wa mkoa wa Geita, Magalula Said pamoja na kukiri kutoa agizo la kukamatwa kwa wawekezaji hao alikanusha sababu zilizotolewa na uongozi wa TACOGA walizodai ni kutokana na kutokujiunga na mpango wa kilimo cha mkataba na kuongeza kuwa wawekezaji hao walikamatwa kutokana na kitendo chao cha kukiuka utaratibu wa usambazaji wa pembejeo za kilimo katika upande wa viuatilifu ambapo walitakiwa kuvisambaza kwa wakulima kwa njia ya mkopo na siyo kuwauzia kwa fedha taslimu.



Mmoja wa wawakilishi wa makampuni hayo alithibitisha kukamatwa kwao na kuwekwa mahabusu ya polisi kwa zaidi ya masaa manne ambapo hata hivyo alisema baadae waliachiwa huru baada ya polisi kukosa shitaka la kuwafungulia ili kuweza kuwafikisha mahakamani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post