VILABU VYA POMBE NOMAAAA!......NYAMA YA FISI YALIWA KAMA MBUZI


WATU wawili akiwamo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ihumwa, Kata ya Mtumba mjini Dodma wamekutwa wakiuza nyama ya fisi kwenye kilabu cha pombe za kienyeji.

Wanaotuhumiwa kuuza nyama hiyo ni Mwenyekiti, Gabriel Mwaluko na Dickson Mafutaa aliyekuwa akishirikiana naye katika biashara ya ‘kitoweo’ hicho.

Kukamatwa kwa watu hao kulitokana na taarifa za wananchi zaidi ya 10 walionunua na kula nyama hiyo na kuingiwa wasiwasi kutokana na kuuzwa kwa bei rahisi, hali ambayo ilifanya wafikishe taarifa hiyo kwa Ofisa Afya.

Akizungumzia tukio hilo la Jumatatu mchana, Ofisa Afya wa Kata ya Mtumba, Michael Dong’o alisema Mwenyekiti huyo alikutwa ameweka nyama hiyo kwenye mifuko ya nailoni maarufu kama Rambo na kuiuza kati ya Sh 500 hadi Sh 1,000 kwa kipande.

Dong’o alisema baada ya kumhoji alidai nyama waliyokuwa wakiuza ilitokana na fisi waliyemwua kutoka kwenye pori la Ihumwa. Alisema walimchuna na kukata vipande vya nyama na kuipeleka kwenye kilabu cha pombe za kienyeji kuuza.

Kwa mujibu wa Ofisa Afya, watuhumiwa hao walikiri kuuza nyama ya fisi na wakati huo huo inadaiwa walikutwa na ngozi ya mnyama huyo ikiwa imehifadhiwa kwenye mfuko wa plastiki.

Ofisa Afya alidai Mwenyekiti huyo wa kitongoji alisema licha ya kuuza nyama hiyo kilabuni, pia familia yake ilipata. Ofisa huyo alitaka watu kuwa makini kwa kujihadhari na kula nyama zilizothibitishwa na wataalamu wa afya.

Alisema ni vizuri kwa wananchi kuacha uchu wa kula nyama, hasa zinazouzwa kwenye vilabu vya pombe za kienyeji kuepuka magonjwa hatari yanayoweza kusababishwa na nyama.

Kulingana na maelezo ya Ofisa huyo, wanakusudia kuwafungulia watuhumiwa hao mashitaka kwa ajili ya uchunguzi zaidi na hata uhalali wa kuwa na nyama na ngozi ya fisi.

Walaji wahadharishwa
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Benedict ole Nangoro, amehadharisha walaji wa nyama kujenga utamaduni wa kufuatilia wanachokula hasa nyama.

Ametaka hilo lifanyike kubaini sehemu inakochinjwa kwa lengo na kujiridhisha na ubora wa nyama badala ya kununua buchani peke yake.

Akifungua mkutano wa tano wa Baraza la Mwaka la Wadau wa Tasnia ya Nyama nchini jana, Naibu Waziri alisema hatua hiyo itabana wafanyabiashara wasio waaminifu kwenye sekta hiyo kuchanganya nyama ya ng’ombe na nyingine zinazoweza kusababishia walaji madhara.

Alisema sheria ya ufuatiliaji iko wazi ingawa hakutaja inasemaje.

Ulaji nyama chini
Akielezea kiwango cha ulaji nyama nchini, Nangoro alisema utafiti umebaini kuwa licha ya Tanzania kuwa na idadi kubwa ya mifugo, ulaji nyama kwa wananchi wake ni wa chini.

Alisema ulaji huo kwa Mtanzania ni wastani wa kilo 12 kwa mwaka, tofauti na kiwango kilichopendekezwa na Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa wa kilo 50 kwa mtu kwa mwaka.

Aliongeza kuwa machinjio na sehemu ya kuuzia nyama ni duni na hivyo kusababisha kupoteza soko la ndani na kulazimu Serikali kuagiza nyama kutoka nje ya nchi.

Kwa mujibu wake, kati ya Januari na Februari mwaka huu, nyama iliyoingizwa nchini ilikuwa tani 192 za ng’ombe, 8.2 kondoo na tani 48.5 za nguruwe; thamani ya tani hizo ni takribani Sh bilioni 1.3.

Alisema kinachosikitisha zaidi ni ukweli kwamba sehemu kubwa ya nyama hiyo inatokana na mifugo inayozalishwa nchini.

“Mifugo hii inasafirishwa nchi jirani kwa njia haramu na kusindikwa na kurudishwa nchini kama nyama iliyoagizwa kutoka nje na kuuzwa bei kubwa,” alisema.

Alieleza: “Hii inatokana na kutotumia uwezo wote wa machinjio ya kisasa na kutokuwa na majokofu maalumu yenye uwezo wa kupooza nyama hadi nyuzi joto -40 na pia kutokuwa na uwekezaji mkubwa katika biashara ya mifugo, kusindika na kuuza”.

Takwimu zinaonesha nchini kuna ng’ombe milioni 22.8 , mbuzi milioni 15.6, kondoo milioni 7.0, nguruwe milioni 2.01 , kuku wa asili milioni 35.5 na wa kisasa milioni 24.5.

Zaidi ya asilimia 90 ya nyama inayozalishwa nchini, ilitajwa na Naibu Waziri kwamba inatokana na machinjio yanayomilikiwa na mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo kwa asilimia kubwa hazikidhi viwango vya usafi na kutaka wahusika kuziboresha kufikia viwango vinavyokubalika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments