Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAWILI WAKAMATWA KWA MAUAJI YA DEREVA BODABODA NAMTUMBO


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma SACP Marco G Chilya akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 12 juni 2026 Makao makuu ya Polisi Mkoa wa Ruvuma Kamanda Chilya akiwa ameshika moja ya madumu ya mafuta aina ya petrol yaliyokamatwa na jeshi la polisi Mkoani Ruvuma yenye jumla ya madumu 153 zenye lita 3260 zenye thamani ya shilingi milioni 13,916,940 yakisafirishwa kwenda nchi jirani kwa kutumia gari aina ya Canter yenye namba za usajili T.881 BRA .
























Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma 


Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma limewakamata watuhumiwa wawili kwa tuhuma za kumuua dereva bodaboda, Husein Komoro Matiri (22), mkazi wa Rwinga wilayani Namtumbo, na kupora pikipiki yake yenye namba za usajili MC 273 EQV aina ya HAOJUE. 


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, SACP Marco G. Chilya, ameeleza hayo leo Juni 12, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari.


Kamanda Chilya amesema mwili wa marehemu ulipatikana Mei 30, 2026 katika mashamba ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilayani Namtumbo ukiwa na jeraha la kupigwa kwa kitu kizito na butu kwenye paji la uso.


 Baada ya mauaji hayo, wahalifu waliondoka na pikipiki yake.


Amesema uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi umefanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa wawili wanaohusishwa na tukio hilo, huku juhudi za kurejesha mali iliyoporwa na kubaini washirika wengine zikiendelea.


Kamanda Chilya amesema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.


 Aidha, ametoa onyo kwa wahalifu wanaojihusisha na matukio ya mauaji na uporaji dhidi ya waendesha bodaboda kuacha mara moja vitendo hivyo.


Pia ametoa rai kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za uhalifu na kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi, akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi halitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya uhalifu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com