Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

POLISI RUVUMA WABAINI WIZI WA BETRI ZA TANESCO NA UHUJUMU WA UMEME WA MILIONI 32.
















Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma 


Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma linawashikilia watu kadhaa, akiwemo mhasibu, fundi na walinzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa betri 28 za volti 12 aina ya DRYCELL zenye thamani ya Sh milioni 32.4 zilizokuwa zimehifadhiwa katika ofisi kuu za shirika hilo kwa matumizi ya dharura.


Akizungumza na waandishi wa habari Juni 12, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, SACP Marco G. Chilya, amesema watuhumiwa hao wanashikiliwa wakati uchunguzi ukiendelea, na watafikishwa mahakamani mara uchunguzi utakapokamilika. 


Betri hizo ni mali ya TANESCO Mkoa wa Ruvuma na zilikuwa zikihifadhiwa kama mfumo wa akiba ya umeme (backup batteries).


Katika tukio jingine, polisi walimkamata Tumaini Marunda Kirra (41), mfanyabiashara wa eneo la Kuchire-Msamala, Songea, kwa kujiunganishia umeme kinyume cha sheria kwa kutumia mfumo uliokuwa haupitii kwenye mita ya umeme. 


Kitendo hicho kilisababisha TANESCO kupata hasara ya Sh milioni 18.7 kwa kipindi cha miaka miwili.


Kamanda Chilya amesema baada ya mahojiano ya kina, mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na tukio hilo na kulipa faini ya Sh milioni 18.7 kwa mujibu wa taratibu za shirika.


 Aidha, watu wawili wengine wamekamatwa wakiwa na lita 3,260 za petroli zenye thamani ya Sh milioni 13.9 zilizokuwa zikisafirishwa kwenda nchi jirani kinyume cha sheria kwa kutumia gari aina ya Canter yenye namba T 881 BRA.


Mbali na hayo, Kamanda Chilya amewataka wananchi kuepuka vitendo vya kuhujumu miundombinu ya serikali na badala yake kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika.


 Amesisitiza kuwa uharibifu wa miundombinu hiyo husababisha hasara kubwa kwa serikali na wananchi, kwani fedha zinazotumika kuijenga na kuitunza hutokana na kodi za Watanzania.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma SACP Marco G Chilya Madumu ya mafuta aina ya petrol yaliyokamatwa na jeshi la polisi Mkoani Ruvuma yenye jumla ya thamani ya shilingi milioni 13,916,940 yakisafirishwa kwenda nchi jirani kwa kutumia gari aina ya Canter yenye namba za usajili T.881 BRA. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com