Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limewapa nafasi ya pili vijana waliochaguliwa kujiunga na mafunzo kwa mujibu wa sheria mwaka 2026 lakini wakashindwa kuripoti katika makambi waliyopangiwa, kwa kuwaelekeza kufika katika makambi yaliyo karibu na maeneo wanayoishi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mkuu wa Tawi la Mafunzo la JKT, Brigedia Jenerali Peter Mnyani, amesema uamuzi huo umetokana na dhamira ya kuhakikisha hakuna kijana anayekosa fursa ya kushiriki mafunzo kutokana na changamoto mbalimbali zilizomzuia kuripoti awali.
Amesema vijana wote waliokosa kuripoti katika makambi yao ya mwanzo wanapaswa kuwasili katika makambi ya JKT yaliyo karibu nao ili kupokelewa na kuanza mafunzo.
Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Mnyani, makambi yaliyotengwa kwa ajili ya kuwapokea vijana hao ni Kambi ya Ruvu JKT mkoani Pwani, Kambi ya Makutupora JKT mkoani Dodoma pamoja na Chuo cha Uongozi cha JKT (CUJKT) kilichopo Kimbiji jijini Dar es Salaam.
Amefafanua kuwa zoezi la kuripoti litafanyika kuanzia Juni 12 hadi Juni 15, 2026, huku akiwataka vijana wote wenye sifa kutumia fursa hiyo kwa wakati ili kutimiza wajibu wao wa kushiriki mafunzo ya JKT.

Social Plugin