Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BRELA WAHIMIZA WAFANYABIASHARA KURASIMISHA BIASHARA ZAO



Na. Wellu Mtaki, Dodoma.

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA ) amewahimiza wafanyabiashara ambao bado hawajarasimisha biashara zao kutumia fursa ya maonesho kupata elimu na huduma mbalimbali huku akisisitiza kuwa urasimishaji wa biashara ni hatua muhimu inayochochea ukuaji wa biashara na kufungua fursa za maendeleo.

Meyasema hayo Afisa Usajili wa BRELA, Yusufu Mwasagafuka wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma katika maonesho ya wiki ya utumishi yanayofanyika jijini hapo huku akisema zaidi ya wananchi 200 wametembelea Banda hilo ikiwa zaidi ya watu 50 wakifanikiwa kupata vyeti vya usajili wa majina ya biashara papo kwa papo.

Amesema mwitikio wa wananchi tangu kuanza kwa maonesho hayo umekuwa mkubwa, jambo linalodhihirisha ongezeko la uelewa kuhusu umuhimu wa urasimishaji wa biashara.

Aidha Amesema kuwa wananchi wanaofika katika banda hilo wanapata huduma mbalimbali ikiwemo usajili wa kampuni, usajili wa majina ya biashara, utoaji wa leseni za biashara pamoja na huduma za ushauri kuhusu masuala mbalimbali ya usajili.

"Tangu tulipoanza kushiriki maonesho haya tumepokea wananchi wengi wanaohitaji huduma na ufafanuzi kuhusu changamoto wanazokumbana nazo katika matumizi ya mifumo ya usajili. Tunawakaribisha wananchi zaidi kufika katika banda letu ili kupata huduma na taarifa sahihi," amesema.

Sambamba na hayo amefafanua kuwa BRELA inasimamia huduma mbalimbali zikiwemo usajili wa makampuni, majina ya biashara, alama za biashara, hataza, leseni za viwanda na leseni za Kundi A.

Amebainisha kuwa pamoja na maboresho yanayoendelea kufanywa katika mifumo ya usajili, baadhi ya wananchi bado wanakumbana na changamoto zinazotokana na kutokumbuka taarifa walizotumia wakati wa usajili wa awali.

"Baadhi ya wateja wanapofika kupata huduma wanashindwa kukumbuka namba za simu, anuani za barua pepe au taarifa nyingine walizowasilisha wakati wa usajili wa mwanzo hii husababisha ugumu katika uhakiki wa taarifa na upatikanaji wa huduma kwa wakati," amesema.

"Urasimishaji wa biashara ndiyo msingi wa ukuaji wa biashara. Kupitia BRELA, wafanyabiashara wanapata utambulisho rasmi unaowawezesha kupanua shughuli zao na kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi," amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com