
Na Kadama Malunde, Shinyanga
Wadau wa sekta ya maji katika Mkoa wa Shinyanga wamepitisha na kuidhinisha mapendekezo ya marekebisho ya bei za huduma za maji safi na usafi wa mazingira yaliyowasilishwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), huku Serikali ikisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuhakikisha utekelezaji wa mabadiliko hayo unafanyika kwa uelewa na ushirikiano wa jamii.
Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha wadau kilichofanyika Juni 2, 2026 katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na kuongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita, kikihusisha viongozi wa serikali, vyama vya siasa, madiwani, wadau wa maendeleo, sekta binafsi na wananchi.
Akiwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya bei, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa SHUWASA, Reuben Mwandumbya, amesema hatua hiyo inalenga kuiwezesha mamlaka kuendelea kutoa huduma bora, salama na endelevu kwa wananchi huku ikikabiliana na changamoto za ongezeko la gharama za uendeshaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira.
Ameeleza kuwa marekebisho hayo yatasaidia kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama, kuboresha miundombinu ya uzalishaji na usambazaji wa maji, kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wateja pamoja na kuwezesha utekelezaji wa miradi mipya ya upanuzi wa huduma katika maeneo mbalimbali yanayohudumiwa na SHUWASA.
"Kwa mujibu wa viwango vipya vitakavyoanza kutumika katika mwaka wa fedha 2026/27, wateja wa majumbani wanaotumia zaidi ya mita za ujazo tano kwa mwezi watalipa Shilingi 1,840 kwa mita ya ujazo kutoka Shilingi 1,740 za sasa.
Taasisi mbalimbali zitalipa Shilingi 3,060 kwa mita ya ujazo kutoka Shilingi 2,760, huku wateja wa sekta ya biashara wakiongezeka kutoka Shilingi 2,790 hadi Shilingi 3,100 kwa mita ya ujazo",ameeleza Mwandumbya.
Aidha, amebainisha kuwa, gharama za huduma ya maji kwa viwanda zimeongezeka kutoka Shilingi 2,850 hadi Shilingi 3,160 kwa mita ya ujazo, wakati viwanda vya vinywaji vitatozwa Shilingi 4,160 kutoka Shilingi 3,750 za awali. Kwa upande wa vibanda vya kuuza maji, kiwango kipya kitakuwa Shilingi 1,670 kwa mita ya ujazo kutoka Shilingi 1,500 zilizokuwa zinatumika hapo awali.
Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya SHUWASA, Reuben Kitinya, amesema mabadiliko hayo yametokana na kupanda kwa gharama za mabomba, viungio, madawa ya kutibu maji, vifaa vya uendeshaji na matengenezo ya miundombinu ya maji pamoja na mahitaji yanayoongezeka ya wananchi ya kupata huduma bora.
Amesema lengo la marekebisho hayo si kuwaongezea wananchi mzigo usio wa lazima, bali kuiwezesha SHUWASA kuendelea kutoa huduma endelevu, salama na yenye ubora unaokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.
“Maji safi ni hitaji la msingi kwa maisha ya binadamu, afya ya jamii, maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa mazingira. Ni wajibu wetu kuhakikisha miundombinu ya maji inalindwa, inaboreshwa na kupanuliwa ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na huduma hizi muhimu,” amesema Kitinya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola, amesema mamlaka hiyo imeendelea kutekeleza majukumu yake ya kutoa huduma za maji katika Manispaa ya Shinyanga pamoja na maeneo ya Tinde, Didia na Iselamagazi huku ikiendelea kuboresha mifumo ya utoaji huduma.
Amesema bei zilizokuwa zinatumika zimekaa kwa muda mrefu bila kufanyiwa marekebisho wakati gharama za ununuzi wa maji ya jumla, madawa ya kutibu maji, ukarabati wa miundombinu na shughuli nyingine za uendeshaji zimeendelea kuongezeka.
Baada ya majadiliano ya kina, wadau wamekubaliana na kupitisha mapendekezo hayo, wakieleza kuwa viwango vipya vimeidhinishwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria na vimetangazwa rasmi kupitia Gazeti la Serikali, jambo linalovipa uhalali wa kiudhibiti na kisheria katika utekelezaji wake.
Baada ya kupitisha viwango hivyo, pia wadau wameweka maazimio kadhaa muhimu ikiwemo kuendelea kubaki kwa bei ya maji yanayouzwa katika magati kwa Shilingi 50 kwa ndoo ili kulinda uwezo wa wananchi wa kipato cha chini kupata huduma ya maji kwa gharama nafuu.
Wadau hao pia wamesisitiza umuhimu wa SHUWASA kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya maji, umuhimu wa kulipia huduma kwa wakati na sababu za mabadiliko ya bei ili kuondoa sintofahamu zinazoweza kujitokeza kabla ya viwango vipya kuanza kutumika Julai 1, 2026.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita, ameipongeza SHUWASA kwa juhudi zake za kuendelea kuboresha huduma za maji na kusisitiza kuwa elimu kwa wananchi inapaswa kuendelea kutolewa kwa nguvu kubwa ili jamii ielewe sababu za mabadiliko hayo na manufaa yatakayopatikana.
Mtatiro amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwekeza mabilioni ya shilingi katika miradi ya maji nchini kwa lengo la kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inawafikia wananchi wengi zaidi mijini na vijijini.
Ameeleza kuwa serikali itaendelea kusogeza huduma za maji karibu na wananchi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati, huku taasisi za utoaji huduma zikihimizwa kuongeza uwazi, uwajibikaji na mawasiliano ya karibu na wananchi.
“Ni muhimu wananchi wakapata elimu ya kutosha kuhusu mabadiliko haya ili waelewe kuwa lengo lake ni kuboresha huduma. Wakati huo huo, taasisi husika ziendelee kuhakikisha uwekezaji unaofanywa na Serikali unaleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi kupitia upatikanaji wa maji wa uhakika,” amesisitiza Mtatiro.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, wakati wa kikao cha wadau wa maji kilichoandaliwa na SHUWASA kujadili na kupitisha mapendekezo ya marekebisho ya bei za huduma za maji na usafi wa mazingira. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, wakati wa kikao cha wadau wa maji kilichoandaliwa na SHUWASA kujadili na kupitisha mapendekezo ya marekebisho ya bei za huduma za maji na usafi wa mazingira.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, wakati wa kikao cha wadau wa maji kilichoandaliwa na SHUWASA kujadili na kupitisha mapendekezo ya marekebisho ya bei za huduma za maji na usafi wa mazingira.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, wakati wa kikao cha wadau wa maji kilichoandaliwa na SHUWASA kujadili na kupitisha mapendekezo ya marekebisho ya bei za huduma za maji na usafi wa mazingira.
Baadhi ya wadau wa sekta ya maji mkoani Shinyanga wakifuatilia kwa makini majadiliano kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya bei za huduma za maji na usafi wa mazingira yaliyowasilishwa na SHUWASA.
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola, akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa maji, ambapo ameeleza mikakati ya mamlaka hiyo ya kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola, akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa maji, ambapo ameeleza mikakati ya mamlaka hiyo ya kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya SHUWASA, Reuben Kitinya akizungumza kwenye kikao cha wadau wa maji
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa SHUWASA, Reuben Mwandumbya, akiwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya bei ya huduma za maji.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog






















































































Social Plugin