Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WENYE MAHITAJI MAALUM KUPEWA KIPAUMBELE MAFUNZO YA JKT



Na Dotto Kwilasa, Dodoma 

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limesema vijana wenye mahitaji maalum, hususan wenye ulemavu wa viungo, wamewekewa mazingira rafiki yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu mafunzo ya uzalendo na stadi za maisha yanayoanza rasmi Juni mwaka huu.

Hatua hiyo imekuja sambamba na maandalizi ya kupokea jumla ya vijana 60,000 wa kidato cha sita kutoka shule mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar watakaoripoti katika makambi ya JKT kuanzia Juni 1 hadi Juni 7, 2026.

Akizungumza jijini Dodoma leo Mei 28, 2026 kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele, Mkuu wa Utawala wa JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema vijana wenye mahitaji maalum watapangiwa katika Kambi ya Ruvu mkoani Pwani kutokana na uwepo wa miundombinu na huduma zinazokidhi mahitaji yao.

Amesema Serikali imeendelea kuboresha mfumo wa mafunzo hayo kwa kuongeza idadi ya vijana wanaopokelewa kutoka 40,000 hadi 60,000 mwaka huu ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uzalendo, nidhamu na uwezo wa kujitegemea kwa vijana.

“Lengo ni kuwajenga vijana kuwa na maadili mema, uzalendo na stadi zitakazowasaidia katika maisha yao ya baadaye na katika kulitumikia taifa,” amesema Mabena.

Kwa mujibu wa Mabena, vijana hao watapangiwa katika makambi mbalimbali nchini ikiwemo Rwamkoma Mara, Msange Tabora, Mpwapwa na Makutupora Dodoma, Mafinga Iringa pamoja na Oljoro Arusha.

Makambi mengine yaliyotajwa ni Bulombora Kagera, Kanembwa na Mtabila Kigoma, Itaka Songwe, Luwa na Milundikwa Rukwa pamoja na Nachingwea mkoani Lindi.

Aidha, JKT limewataka vijana wote waliochaguliwa kuzingatia maelekezo ya kuripoti kwa wakati pamoja na kubeba vifaa muhimu vitakavyotumika wakati wa mafunzo, ikiwemo mavazi ya michezo, shuka, soksi na nyaraka muhimu za masomo na utambulisho.

Amesema mafunzo hayo hayalengi kuwapa vijana maarifa ya kijeshi pekee, bali pia kuwaandaa kuwa raia wenye nidhamu, uwezo wa kufanya kazi na kujitegemea hata kwa wale watakaokosa nafasi za kuendelea na elimu ya juu.

Programu ya mafunzo ya lazima ya JKT ilirejeshwa rasmi mwaka 2013 ikiwa na dhamira ya kuwajengea vijana moyo wa uzalendo na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com