
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar Es Salaam limesema linaendelea kupeleleza kwa uzito mkubwa tukio la mauaji ya Bw. James Rogers Temba, mwanafunzi wa mwaka wa pili kutoka Chuo cha cha IFM Jijini Dar Es Salaam ambaye mwili wake ulikutwa unaelea kwenye maji yaliyokuwa yanatiririka katika Mto Msimbazi eneo la Kipawa, Wilayani Ilala mnano Aprili 30, 2026 ukiwa hauna kichwa.
Kamanda wa Polisi Kanda maalumu ya Dar Es Salaam, SACP Jumanne Muliro amewaambia waandishi wa habari leo Jumatano Mei 06, 2026 kuwa tayari wamewakamata watuhumiwa wanne akiwemo Steven Chaka (31), afisa maabara mkazi wa Bomang'ombe, Hai, Mkoani Kilimanjaro na Anna Frank Lema (30), mfanyabiashara na mkazi wa Tabata Chang'ombe Jijini Dar Es Salaam.
"Wengine ni Twalibu Khamis Mpulo (23) mkazi wa Kigogo Kati Jijini Dar Es Salaam pamoja na Michael John (26) mkazi wa Kigogo, Jijini Dar Es Salaam. Vipo pia baadhi ya vielelezo ambavyo vinachunguzwa kuhusiana na tukio hilo." Amesema Kamanda Muliro.
Katika hatua nyingine Polisi imetoa wito kwa wananchi kuendelea kuwa watulivu ili kila anayehusika kulingana na ushahidi aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Social Plugin