
Boaz Martine enzi za uhai wake

Eneo la ajali
Na Kadama Malunde - Shinyanga
Mpiga picha wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Boaz Martine, amefariki dunia huku waandishi wa habari Frank Mshana wa ITV/Radio One na Johnson James wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga wakiwa miongoni mwa watu saba waliojeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea Mei 19, 2026 eneo la Samuye/Usanda wilayani Shinyanga.
Ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Toyota Harrier lenye namba T.210 EDB na Toyota Land Cruiser Hardtop lenye namba DFPA 8920 mali ya KOICA, lililokuwa limebeba waandishi wa habari pamoja na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga wakitokea ziara ya Tinde.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 20, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa Toyota Harrier aliyekuwa akijaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake bila tahadhari na kusababisha kugongana na Land Cruiser hiyo iliyotumbukia mtaroni.
Majeruhi wengine ni Koplo Swahiba Msangi, Neema Madono (36), Rehema Edson (45), Shadia Omari (32) pamoja na dereva wa Land Cruiser, Laurence Peter (34), ambao wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Mwenyekiti wa MISA Tanzania Edwin Soko amesema taasisi hiyo inasikitishwa na ajali hiyo iliyowahusisha wanachama wake Frank Mshana wa ITV na Johnson James wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, huku akitoa pole kufuatia kifo cha Boaz Martine na kuwaombea majeruhi wote wapate nafuu haraka.
Mazishi ya marehemu Boaz Martine, yanatarajiwa kufanyika Alhamisi Mei 21, 2026 katika makaburi ya familia yaliyopo Mwawaza, Manispaa ya Shinyanga.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawala na Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, David Lyamongi, ibada ya kumuombea marehemu itaongozwa na Mashahidi wa Yehova kuanzia saa 7:00 mchana nyumbani kwa marehemu nyuma ya Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Kitangili, Manispaa ya Shinyanga.
Baada ya ibada na salamu za rambirambi, mwili wa marehemu utapelekwa katika makaburi ya familia yaliyopo Mwawaza kwa ajili ya mazishi yatakayoanza majira ya saa 9:00 alasiri
Social Plugin