Wakati mamilioni ya Wakristo nchini Tanzania leo wameungana na ulimwengu mzima kuadhimisha Sikukuu ya Pasaka, viongozi wa kiroho wametoa ujumbe mzito wakitaka Taifa kurejea katika misingi ya utu.
Katika mfululizo wa mahubiri ya kukumbuka ufufuo wa Yesu Kristo, viongozi hao wameelezea wasiwasi wao juu ya kuporomoka kwa maadili, huku wakikemea vikali tabia ya baadhi ya wananchi kusherehekea vifo vya viongozi na kuukumbatia uongo badala ya ukweli.
Katika kile kinachoonekana kama mwito wa kurekebisha mshikamano wa kijamii, viongozi hao wamesisitiza kuwa mwenendo wa sasa nchini ni dalili ya hatari ya kupotea kwa misingi ya utu.
Wameonya kuwa, wakati wananchi wanapaswa kurejea kwenye ukweli, wale waliopo madarakani nao wanapaswa kutumia wakati huu wa Pasaka kujitafakari kwa kina kuhusu namna wanavyoongoza na kuishi na wale wanaowaongoza ili kuziba nyufa zinazojitokeza katika jamii.
Akizungumza kwa hisia kali, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bagamoyo, Mhashamu Stephano Lameck Musomba, amelaani kitendo cha baadhi ya watu kushangilia vifo vya viongozi, akitaja hali hiyo kama kovu kubwa la kimaadili.
Akihubiri katika Parokia ya Bikira Maria wa Mlima wa Karmeli, Bunju jijini Dar es Salaam, Askofu Musomba amebainisha kuwa hali hiyo si ya kawaida na inaashiria kuwepo kwa matatizo ya kijamii yanayohitaji kutazamwa kwa jicho la ziada, badala ya kuyapuuza.
Askofu Musomba amelikumbusha Taifa kuwa, kwa mujibu wa mila na desturi za Kiafrika, kifo ni tukio la huzuni na mshikamano, si jambo la dhihaka au ushindi.
Ameeleza kuwa mabadiliko haya ya tabia ni kengele ya hatari inayoashiria kuporomoka kwa misingi ya uungwana na ubinadamu iliyolijenga Taifa la Tanzania kwa miaka mingi. Ametoa wito wa kuwepo kwa majadiliano ya dhati na uvumilivu wa kisiasa ili kupunguza tofauti zinazoweza kusababisha chuki miongoni mwa wananchi.
Ili kunusuru mshikamano wa nchi, kiongozi huyo wa kiroho amewataka Watanzania kuelimishana na kutafuta haki kwa njia za amani na sahihi.
Amesema kuwa bila juhudi za makusudi za kurejesha haki na utu, jamii ipo hatarini kuingia katika migogoro isiyo ya lazima na kupoteza mwelekeo wa kitaifa. Aidha, amekemea kuongezeka kwa imani za kishirikina ambazo zimekuwa zikichangia uvunjifu wa amani na kuzorotesha maendeleo katika baadhi ya maeneo nchini.

Social Plugin