
Na Hadija Bagasha - Tanga
Viongozi wa dini kote nchini wakiwemo Maaskofu wametakiwa kuhakikisha wanatumia majukwaa yao ya kidini kuhubiri masuala ya amani, upendo na mshikamano badala ya kuhubiri mambo yanayoleta uchonganishi yanayoweza kugawa jamii na kutengeneza chuki miongoni mwao.
Hayo yamesemwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la The Free Pentecostal Church of Tanzania (FPCT), Tanzania Stivie Mulenga wakati wa ibada maalum ya Pasaka iliyofanyika kanisani hapo jijini Tanga.
Amesema kuwa ibada zinapaswa kubaki kuwa mahali pa kumtukuza Mungu, siyo jukwaa la kuwashambulia au kuwapendelea watu fulani.
Katika mahubiri yake yaliyojaa msisitizo wa maadili na mshikamano wa kijamii, alikumbusha kuwa msingi wa imani ya Kikristo ni amani, siyo migawanyiko.
Ameeleza kuwa Yesu Kristo hakuja duniani kuleta chuki au uchonganishi, bali alikuja kuleta upendo na amani miongoni mwa wanadamu.
Aidha, amesema kuwa kufufuka kwake ni ishara ya ushindi wa amani juu ya giza, hivyo viongozi wa dini wanapaswa kuendeleza urithi huo kwa vitendo na maneno yao.
“Ni muhimu sana kwa viongozi wa dini kutambua uzito wa majukwaa waliyonayo. Wanaposimama kuhubiri, wanapaswa kuwajenga watu katika misingi ya upendo, uvumilivu na kuchukuliana, badala ya kueneza maneno yanayoweza kuleta mifarakano,” amesisitiza Mulenga.
Askofu huyo pia amegusia umuhimu wa kuheshimu misingi ya taifa, akieleza kuwa ingawa serikali haina dini, wananchi wake wana uhuru wa kuabudu na kuishi kwa mujibu wa imani zao bila kuvunja sheria.
Amepongeza hali hiyo ya uhuru wa kuabudu akisema ni jambo la kujivunia na kulindwa kwa nguvu zote.
Ameonya kuwa kipindi cha Pasaka kisitumike kama kichocheo cha fitina au vurugu, bali kiwe fursa ya kujenga upya mahusiano ya kijamii na kuimarisha mshikamano.
Mbali na hilo, Askofu Mulenga ameeleza wasiwasi wake kuhusu mmomonyoko wa maadili unaoonekana katika jamii, akitaja tamaa binafsi kuwa chanzo kikubwa cha matatizo mengi yanayotokea hata kushangaza ulimwengu.
Amewataka viongozi wa dini kuongeza juhudi katika kuwaelimisha waumini juu ya maadili mema na kujiepusha na vitendo viovu.
Amehamasisha pia umuhimu wa kupinga ukatili wa kijinsia, akiwataka viongozi wa dini kuwa mstari wa mbele katika kuelimisha jamii na kulaani vikali vitendo hivyo. Kwa mujibu wake, jamii yenye maadili na heshima ndiyo msingi wa amani ya kweli na maendeleo endelevu.
Askofu Mulenga ametoa wito kwa kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika kujenga taifa lenye amani na utulivu kwa kuzingatia matendo mema na kuheshimu utu wa kila mmoja.



Social Plugin