
Na Mwandishi wetu - Shinyanga
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka, amewataka vijana wa Mkoa wa Shinyanga kuacha kuwa watazamaji wa masuala ya kiuchumi na badala yake wawe washiriki wakuu katika maendeleo ya mkoa na taifa.
Akizungumza Februari 21, 2026 katika uzinduzi wa Jukwaa la Vijana mkoani humo, amesema serikali imeweka fursa mbalimbali zikiwemo mikopo, mafunzo na teknolojia kwa ajili ya kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi.

“Vijana hawapaswi kuwa watazamaji wa mambo ya uchumi, bali wawe washiriki wakuu. Kwa kutumia fursa za mikopo, ujuzi na teknolojia, mnaweza kuanzisha viwanda vidogo vidogo, kujenga mitandao ya biashara na kujikwamua kiuchumi,” amesisitiza Nanauka.
Ameongeza kuwa mikataba zaidi ya saba imeingiwa kwa ajili ya kuwapeleka vijana kufanya kazi nje ya nchi, huku shilingi bilioni 200 zilizotolewa na Rais zikianza kutumika kama mtaji kwa vijana.
Katika mwaka wa fedha 2024/2025, zaidi ya shilingi bilioni 2 zimetolewa kupitia mikopo ya asilimia 10 katika Mkoa wa Shinyanga, na zaidi ya bilioni 5 kupitia Mfuko wa Utamaduni kusaidia vijana wenye vipaji na ubunifu.
“Ndoto yako ndiyo mtaji wako. Ukiamua jambo lako, usikubali kuyumbishwa. Mafanikio ni fursa kwa aliyejiandaa,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita amesema Shinyanga ina vijana zaidi ya laki 6.9 na tayari zaidi ya wajasiriamali 2,000 wamesajiliwa ili kushiriki rasmi katika shughuli za kiuchumi.
Baadhi ya vijana, akiwemo Elina Evodius na Ebeneza John, wamesema jukwaa hilo limewapa matumaini ya kupata mikopo itakayowawezesha kukuza vikundi na biashara zao.


















Social Plugin