Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHUWASA YATWAA TUZO YA MDAU SHUPAVU KANDA YA ZIWA


Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) imeibuka mshindi wa Tuzo ya Mamlaka Bora inayosimamia upatikanaji wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira katika Tuzo za Wadau Shupavu Kanda ya Ziwa, zilizofanyika Jumatatu tarehe 16 Februari 2026.

Tuzo hiyo ilipokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola, katika hafla iliyofanyika Hoteli ya  Golden Crest, jijini Mwanza.

Akizungumza wakati wa utambulisho, Mhandisi Katopola alisema SHUWASA imetekeleza kwa vitendo jitihada za kumtua mwanamke ndoo kichwani kwa kusogeza huduma karibu na wananchi na kuhakikisha upatikanaji wa majisafi kwa wastani wa saa 23 kila siku.

Aliongeza kuwa juhudi hizo, sambamba na usimamizi madhubuti wa usafi wa mazingira, zimeifanya Manispaa ya Shinyanga kuwa kinara wa usafi kitaifa kwa miaka mitatu mfululizo.

SHUWASA inatoa huduma katika eneo lote la Manispaa ya Shinyanga pamoja na miji midogo ya Didia, Tinde na Iselamagazi, iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. 

Mhandisi Katopola alibainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya Mamlaka na wadau wake, hususan wateja na wananchi, kwa kulipia ankara za maji kwa wakati na kutoa taarifa za uvujaji au uharibifu wa miundombinu.

Aidha Mhandisi Katopola alimshukuru Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Hamidu Aweso kwa maelekezo yake ya mara kwa mara katika kuhakikisha Mamlaka za Maji nchini zinatoa huduma bora za maji safi na usafi wa mazingira kwa wananchi katika maeneo yao ya huduma.

Tuzo hii ni chachu ya kuendelea kuboresha huduma na kudumisha viwango bora vya maji safi na usafi wa mazingira kwa maendeleo ya wananchi wa Tinde, Didia, Iselamagazi na Manispaa ya Shinyanga.  












Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com