Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele akizungumza leo tarehe 24 Januari, 2026 mkoani Iringa wakati akifungua mafunzo ya watendaji wa uchaguzi kutoka Halmashauri za Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma na Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele akizungumza leo tarehe 24 Januari, 2026 mkoani Iringa wakati akifungua mafunzo ya watendaji wa uchaguzi kutoka Halmashauri za Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma na Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe.
Meza Kuu ikiwa katika mafunzo hayo.
****************
Na. Mwandishi Wetu, IringaWatendaji wa uchaguzi wametakiwa kuvishirikisha kwa ukaribu vyama vya siasa vyenye usajili kamili katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi katika maeneo yao ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele leo tarehe 24 Januari, 2026 mkoani Iringa wakati akifungua mafunzo ya watendaji wa uchaguzi kutoka Halmashauri za Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma na Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe.
Mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mdogo wa ubunge kwenye Jimbo la Peramiho lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma na Kata ya Shiwinga iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe unaotarajiwa kufanyika tarehe 26 Februari, 2026.
“Wakati wote wa mchakato wa uchaguzi huu, ni vema mkavishirikisha kwa karibu vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili na wadau wengine wa uchaguzi katika maeneo yenu kuhusu masuala ya kiuchaguzi ambayo wanastahili kushirikishwa kwani jambo hilo litawarahisishia utekelezaji wa majukumu yenu,” amesema Jaji Mwambegele.
Ameongeza kuwa watendaji hao wa uchaguzi wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo watakayopewa na Tume badala ya kufanya kazi kwa mazoea.
“Nachukua nafasi hii kuwaasa kuwa, pamoja na uzoefu ambao baadhi yenu mnao katika uendeshaji wa uchaguzi, mhakikishe mnazingatia maelekezo mtakayopewa na Tume badala ya kufanya kazi kwa mazoea. Kwani kila uchaguzi unatofautiana na uchaguzi mwingine,” amesema.
Amewataka watendaji hao kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum ya vituo husika na kuhakikisha kunakuwa na mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.
Jaji Mwambegele amewasisitiza watendaji hao kuhakikisha wanaajiri watendaji wa vituo wenye sifa, weledi, wanaojitambua na kuachana na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi.
“Mhakiki vifaa vya uchaguzi mnavyopokea kutoka Tume na kuhakikisha kila mkuu wa kituo anapata vifaa vyote vya uchaguzi vinavyohitajika mapema na muweke utaratibu utakaowezesha kila kituo cha kupigia kura kufunguliwa saa 1:00 asubuhi,” amesema.
Aidha, washiriki wa mafunzo hayo kutoka Halmashauri za Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma na Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe walikula viapo vya kujitoa uanachama wa vyama vya siasa na kile cha kutunza siri mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Rehema Mayagilo.
Mafunzo hayo ya siku tatu yamewahusisha Waratibu wa Uchaguzi wa Mikoa ya Songwe na Ruvuma, Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi Ngazi ya Jimbo, Wasimamizi wa Uchaguzi Ngazi ya Kata, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ununuzi na Wahasibu.

Social Plugin