Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika mazishi ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), marehemu Mzee Edwin Isaac Mtei.
Mazishi hayo yamefanyika leo Januari 24, 2026, nyumbani kwa marehemu Tengeru (Chama), Wilaya ya Arumeru Mashariki, Mkoa wa Arusha, yakihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, familia, ndugu, jamaa na wananchi.
Akizungumza katika mazishi hayo, Dkt. Nchemba alisema Rais Samia Suluhu Hassan anatambua na kuthamini mchango mkubwa wa marehemu Mzee Mtei katika ujenzi wa misingi ya uchumi, sekta ya fedha na demokrasia nchini, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuenzi mchango wake kwa vitendo.
Waziri Mkuu alisema marehemu alikuwa miongoni mwa Watanzania wachache waliobahatika kuhudumu katika nyadhifa zote kuu za sekta ya fedha, ikiwemo kuwa Gavana wa BOT, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Waziri wa Fedha pamoja na mwakilishi wa Tanzania katika taasisi za fedha za kimataifa, jambo lililompatia heshima kubwa kitaifa na kimataifa.
Aliongeza kuwa katika maisha yake ya utumishi wa umma, Mzee Mtei alijulikana kwa kusimamia misingi ya uadilifu, uaminifu, uzalendo, bidii na kumcha Mungu, misingi iliyosaidia kujenga taasisi imara za kifedha na nidhamu ya uchumi wa Taifa.
Dkt. Nchemba alibainisha kuwa marehemu pia alikuwa miongoni mwa waasisi wa demokrasia ya vyama vingi nchini, akiwa mwanzilishi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mchango uliosaidia kuimarisha uhuru wa mawazo na mfumo wa kisiasa nchini.
Katika kuenzi mchango wake kwa vitendo, Waziri Mkuu alitoa maelekezo mbalimbali ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara ya njia nne Tengeru–Usa River, kukamilisha usanifu na kuanza ujenzi wa barabara Usa River–KIA, pamoja na ukarabati wa barabara na madaraja katika maeneo korofi kati ya Arusha na Kilimanjaro.
Aidha, alielekeza utatuliwe mgogoro wa ardhi wa Mringa Estate ndani ya mwezi mmoja, akisisitiza haki kwa wananchi waliostahili kunufaika na eneo hilo.
Waziri Mkuu alisisitiza kuwa utekelezaji wa maelekezo hayo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuendeleza maendeleo jumuishi, kusimamia haki za wananchi na kudumisha heshima ya viongozi waliolitumikia Taifa kwa uadilifu, akiwemo Mzee wetu Edwin Isaac Mtei.







Social Plugin