
Na Bora Mustafa, Arusha
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba, ametembelea maeneo ya Katiti, Mahakama ya Mwanzo Maji ya Chai, na kituo cha mafuta cha Total Energy, kufuatia vurugu zilizotokea Oktoba 29 wakati wa uchaguzi.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu alitoa salamu za Mheshimiwa Rais kwa wananchi wa maeneo hayo, akiwatia moyo na kuwahakikishia kuwa serikali ipo pamoja nao katika kuhakikisha maendeleo na utulivu vinarejea.
Pia amesema kuwa amesikitishwa na changamoto wanazopitia wananchi, zikiwemo barabara mbovu na ukosefu wa maji katika baadhi ya maeneo. Amesisitiza kuwa maendeleo hayawezi kufikiwa kama hakutakuwa na amani ya kudumu nchini.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka wananchi kuwa makini dhidi ya uchochezi kutoka kwa watu wasiokuwa raia wa Tanzania, ambao, kwa mujibu wake, wana wivu na ustawi wa nchi. Amesema watu hao wanafanya biashara kupitia machafuko, na hawana maslahi yoyote kwa wananchi wa kawaida.
Kuhusu kituo cha polisi cha Katiti, ambacho kiliharibiwa na kuchomwa moto wakati wa vurugu hizo, Waziri Mkuu amesema serikali imeona umuhimu wa kurejesha huduma hiyo muhimu, kwani wananchi wamekuwa bila kituo cha polisi tangu tukio hilo.
Wakati wa vurugu hizo, kulikuwa na wahalifu wawili waliokuwa wamefungwa katika kituo hicho kwa makosa mazito. Hali hiyo ilionyesha uzito wa athari za vurugu kwa huduma za msingi za ulinzi.
Waziri Mkuu pia amesema kuwa serikali haiwezi kuwataka wananchi waache kutumia kuni kama bado hawajapatiwa gesi. Ameeleza kuwa mradi wa gesi wa Embasai utasaidia maeneo mengi yaliyopangwa kufikiwa kupitia mpango huo.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa Askofu Gwajima aachiwe na aruhusiwe kuendelea na shughuli zake za kiroho kwa waumini wake, kama sehemu ya kuheshimu uhuru wa ibada.
Aidha, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, amesema hakuna mradi wa maji katika maeneo kama Embasai na Maji ya Chai. Amesema wakazi wa Katiti bado hawajapata huduma ya maji ya uhakika.
Mbunge huyo pia amesema wanasikitishwa na kutopatikana kwa huduma ya polisi kutokana na kuharibiwa kwa kituo hicho, na akaomba kituo kipya kijengwe ili kusaidia kuimarisha usalama wa wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Gabriel Makalla, amesema hatarajii kuona tena vurugu kama zile. Aidha, amesema vyombo vya ulinzi na usalama vina jukumu la kuwalinda wananchi na mali zao, huku akisisitiza umuhimu wa utulivu na amani kwa maendeleo ya taifa.



Social Plugin