Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANCCOPS YAJIPANGA KUONGEZA THAMANI YA PAMBA KUPITIA UZALISHAJI WA BIDHAA

Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Mradi wa pamoja wa vyama vikuu vya pamba Tanzania (TANCCOPS), kwa kushirikiana na vyama vikuu vyote wanachama wake, umeshauriwa kuangalia njia za kuongeza thamani ya zao la pamba kwa kuanzisha viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali zitokanazo na zao hilo.

Bidhaa hizo zinaweza kujumuisha mafuta ya pamba, majora, nyuzi, pamba za hospitalini na mashudu kwa ajili ya chakula cha mifugo, hatua ambayo itaongeza thamani ya pamba, kuongeza tija kwa mkulima mmoja mmoja na kuboresha mapato ya vyama vyao kwa ujumla.

Mrajisi Msaidizi wa Vyama Vikuu vya Ushirika mkoa wa Shinyanga, Ibrahim Kakozi, ametoa ushauri huo alipotembelea banda la TANCCOPS LTD katika Maonesho ya Nanenane Jijini Dodoma, akisisitiza umuhimu wa kuharakisha mchakato huo.

Kakozi amesema TANCCOPS inapaswa kuwawezesha vyama vyote 13 vilivyo chini yake kupata ujuzi wa kuongeza thamani ya mazao yao ili kuweza kuzalisha bidhaa zitakazoongeza kipato, kukuza uchumi wa taasisi na kuimarisha maisha ya wanachama wake.

Aidha, ameongeza kuwa sekta ya kilimo kupitia zao la pamba nchini, inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya viwanda na ajira, sambamba na kupunguza utegemezi wa kuuza pamba ghafi kwenda nje ya nchi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com