
Na Mwandishi wetu Malunde 1 blog
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), CPA Juma Kimori, ameonesha dhamira thabiti ya kuendeleza sekta ya kilimo na ushirika nchini.
Akiwa ameambatana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, CPA Jeremiah J. Mugeta, pamoja na viongozi wengine waandamizi, CPA Kimori ametembelea banda la TANNCOPS katika Kijiji cha Ushirika, viwanja vya Nanenane Nzuguni, jijini Dodoma.
Ziara hiyo imelenga kutathmini mchango wa wadau katika sekta ya kilimo, kujadili fursa za ushirikiano wa kimkakati na kutoa mwelekeo wa kitaalamu kwa wakulima wa zao la pamba. Pia, Mwenyekiti Kimori alipata nafasi ya kushuhudia mafanikio ya miradi ya ushirikiano na kuona teknolojia mpya zinazobadilisha taswira ya kilimo nchini.
Maonesho ya Nanenane, yanayotambulika kama jukwaa la kitaifa la kuonesha ubunifu na mafanikio ya sekta ya kilimo na ufugaji, mwaka huu yameibuka na nguvu mpya, yakijumuisha teknolojia za kisasa, bidhaa bora za kilimo na fursa za uwekezaji zinazolenga kuongeza tija na ubora wa mazao.
Kupitia ziara hiyo, CPA Kimori ameonesha dhamira yake katika kukuza na kuboresha matumizi ya teknolojia za kisasa katika kilimo, kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya wadau wa sekta, kuchochea uzalishaji endelevu wa mazao bora, na kuwezesha wakulima wadogo na wakubwa kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.

Social Plugin