Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Kwa heshima kubwa na shamrashamra zilizopambwa na mapokezi ya kihistoria, Dkt. Asha-Rose Migiro amepokelewa rasmi leo Agosti 26, 2025 katika Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) – White House, Dodoma, kama Katibu Mkuu mpya wa CCM.
Mapokezi haya hayakuwa ya kawaida, bali yamebeba uzito wa kihistoria kwani kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa CCM mwaka 1977, nafasi hiyo sasa inashikiliwa na mwanamke.
Wanachama waliokusanyika walionesha furaha na mshikamano mkubwa, wakimpongeza Dkt. Migiro kwa kufikia hatua hiyo adhimu ya kiuongozi.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi, Dkt. Migiro ametoa shukrani za dhati kwa Mwenyekiti wa Chama, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumuamini na kumteua kushika nafasi hiyo nyeti.
Ameeleza kuwa uteuzi huo ni heshima kubwa, lakini pia ni wajibu mzito wa kuendeleza misingi imara ya chama kwa kuzingatia maadili, weledi, na moyo wa kizalendo.
Amesisitiza kuwa yuko tayari kutumikia chama kwa moyo wote, na akatoa wito kwa wanachama wote kushikamana kwa nguvu ili kuhakikisha CCM inapata ushindi mkubwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Dkt. Migiro si mgeni katika nyanja za uongozi,ni mwanazuoni na mwanadiplomasia ambaye amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Waziri wa Sheria na Katiba nchini, na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza.
Uzoefu wake mpana wa kitaifa na kimataifa unampa nafasi ya kipekee ya kuliongoza kwa ufanisi zaidi Baraza Kuu la chama katika kipindi hiki muhimu cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Wengi wanaamini kuwa umahiri wake utakuwa chachu ya mageuzi chanya ndani ya chama na taifa kwa ujumla.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi, amempongeza Dkt. Migiro kwa uteuzi huo na kueleza kuwa ni mtu mwenye maono, uwezo mkubwa wa kiuongozi na anayeelewa vyema siasa za ndani na nje ya nchi.
Nchimbi ametoa shukrani kwa Mwenyekiti wa Chama kwa kumpa nafasi ya kutumikia chama, na kwa wanachama waliompa ushirikiano katika kipindi chake cha uongozi. Sasa, akiwa mgombea mwenza wa Rais Samia, ameahidi kuendeleza ushirikiano wa karibu kwa maslahi ya chama na taifa.
Kwa miaka 48 ya uhai wake, CCM imeongozwa na makatibu wakuu wanaume pekee, lakini sasa sura ya uongozi inabadilika. Kupitia uteuzi huu, Dkt. Migiro ameweka alama isiyofutika – akifungua njia kwa wanawake wengine kushiriki kikamilifu katika siasa na uongozi wa juu wa taifa.
Ni hatua inayobeba matumaini na uthibitisho kuwa wanawake wanaweza kuongoza kwa ufanisi sawa na wenzao wa kiume.
Hatua ya kuwa na Mwenyekiti mwanamke na Katibu Mkuu mwanamke kwa mara ya kwanza katika historia ya chama ni ishara ya mabadiliko makubwa ndani ya CCM na ni ujumbe kwa kizazi kipya kuwa siasa za Tanzania zinaelekea kwenye uwiano na ujumuishaji wa kijinsia kwa vitendo.
Kwa sasa, chama kinaonekana kujiimarisha kwa maono mapya yanayoongozwa na wanawake wawili waliobobea Rais Samia na Dkt. Migiro wawili ambao historia itawakumbuka kama waanzilishi wa sura mpya ya uongozi jumuishi.




Social Plugin