
Na Godwin Myovela, Dodoma
MAMIA ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka ndani ya Jiji na viunga vyake wamemiminika kwa wingi katika Makao Makuu ya chama hicho, wakishuhudia mapokezi ya kihistoria kwa Katibu Mkuu mpya wa CCM, Balozi Dk. Asha-Rose Migiro.
Mamia ya wanachama walipiga nderemo, kushangilia na kuimba nyimbo za hamasa, wakionyesha mshikamano na upendo mkubwa kwa kiongozi wao mpya.
Akizungumza mbele ya umati uliofurika, Dk. Migiro alisema:
“Ndugu zangu, kuja kwangu hapa leo ni matokeo ya mshikamano wenu. Ushirikiano wenu wakati wote nilipokuwa kwenye sekretarieti na kazi tulizozifanya pamoja, ndizo zilizowajengea viongozi wetu imani kwamba ninaweza kurejea tena katika nafasi hii. Waswahili wanasema: kidole kimoja hakivunji chawa.”
Kwa sauti yenye msisitizo, aliendelea kumpongeza mtangulizi wake, Dk. Nchimbi, akisema kazi nzuri aliyofanya chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, na Makamu Wenyeviti Bara na Zanzibar, ndiyo msingi anaouendeleza.
“Nakumbuka Dk. Nchimbi aliingia kwenye chama akiwa kijana mdogo na ameendelea kuwa kada mwaminifu hadi leo. Ninajivunia kurithi kiti chake na kuendeleza kazi nzuri aliyofanya,” alisema huku akishangiliwa na wafuasi.
Aidha, aliushukuru uongozi wa juu wa chama kwa kumwamini, akisisitiza kuwa wanachama wa CCM ndio rasilimali kubwa ya chama.
Dk. Migiro alibainisha kuwa wingi wa wanachama waliomiminika kumlaki ni dalili njema ya maandalizi ya kampeni na ushindi mkubwa kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.
“Kujitokeza kwenu kwa wingi ni dalili nzuri kwa chama chetu na ni uthibitisho kwamba ushindi wa CCM uko karibu,” alisema kwa hamasa kubwa.
Mara baada ya mapokezi hayo, Dk. Emmanuel Nchimbi alimkaribisha rasmi Balozi Migiro, akimsifu kwa sifa na uzoefu wake wa kitaifa na kimataifa.
“Wanachama wa Dodoma ni wakarimu na wameonyesha mshikamano wa kipekee. Kwa mapokezi haya, nakuhakikishia upo kwenye mikono salama,” alisema Nchimbi huku akipigiwa makofi.
Alimpongeza Dk. Migiro kwa historia yake ya kiuongozi, akitaja nyadhifa alizopitia ikiwemo Waziri, Mjumbe wa Kamati Kuu, Mjumbe wa Sekretarieti, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza.
“Hakuna sifa muhimu ambayo Katibu Mkuu wa chama hiki anatakiwa kuwa nayo ambayo wewe huna. Tunamshukuru Mwenyekiti wetu kwa kutambua hilo na kwa kukuteua wewe,” alisisitiza Nchimbi.
Dk. Nchimbi alimgeukia Balozi Migiro na kumtazama kwa dhati, akitamka kwa niaba ya wanachama na taifa lote.
“Tuna imani kubwa nawe, tunaamini utaendeleza mbio hizi kwa kasi na mafanikio makubwa.”
Hapo ukumbi mzima ulilipuka kwa shangwe, nyimbo na hamasa kubwa, ishara ya mshikamano mpya ndani ya chama kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.



Social Plugin