Na Dotto Kwilasa , Dodoma
Mwenendo wa mageuzi katika sekta ya kilimo nchini umepata msukumo mpya baada ya Benki ya Ushirika Tanzania (Coop Bank) kutangaza mikakati kabambe ya kuwainua wakulima kupitia huduma bunifu za kifedha zinazolenga vyama vya ushirika na mnyororo mzima wa thamani ya mazao ya kilimo.
Katika Maonesho ya Kitaifa ya Nanenane 2025 yanayofanyika Nzuguni, Dodoma, Coop Bank imetajwa kuwa miongoni mwa wadhamini wakuu, hatua inayodhihirisha dhamira ya benki hiyo kuwekeza kwa vitendo kwenye kilimo-biashara.
Akizungumza Agosti mosi mwaka huu kwenye maonesho hayo,Mkurugenzi Mtendaji wa Coop Bank, Godfrey Ng’urah, amesema benki hiyo ni ya kipekee nchini kwa kuwa inamilikiwa na wakulima wenyewe kupitia vyama vya ushirika kwa zaidi ya asilimia 51, hivyo kila huduma inayotolewa inalenga moja kwa moja kumsaidia mkulima mdogo na mkubwa kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Huduma zetu zinagusa kila hatua ya kilimo – kutoka mkopo wa pembejeo, ukusanyaji wa mazao, usindikaji hadi uuzaji. Tunahakikisha vyama vya msingi (AMCOS) na vya juu (UNION) vinapata mtaji na msaada wa kitaalamu ili kuongeza tija,” amesema Ng’urah.
Ameeleza kuwa mazao kama kahawa, chai, korosho na ufuta tayari yanapitia mifumo ya ushirika inayosimamiwa na Coop Bank, na kwamba mfumo huu ndio nguzo ya kuhakikisha wakulima wananufaika zaidi na jasho lao.
Benki hiyo ilianza kutoa huduma rasmi Oktoba mwaka jana na kufanyiwa uzinduzi wa kitaifa Aprili mwaka huu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa sasa ina matawi katika Dodoma (makao makuu), Tabora, Kilimanjaro, Mtwara na Moshi, huku ikipanga kupanua huduma nchi nzima.
Katika maonesho ya Nanenane mwaka huu, Coop Bank inawaalika wakulima na wadau wa kilimo kutembelea mabanda yake mawili – moja kwenye eneo la wadhamini wakuu na jingine Kijiji cha Ushirika – ambapo elimu ya kifedha, huduma za mikopo na bidhaa maalum za wakulima zitapatikana.
Maonesho hayo yalifunguliwa na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango yakiongozwa na kaulimbiu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025.”


Social Plugin