NDEJEMBI AWAASA WATUMISHI WA UMMA KULINDA RASILIMALIFEDHA ZINAZOTOLEWA NA RAIS KWA AJILI YA MIRADI YA MAENDELEO

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma katika halmashauri hiyo.
Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa halmashauri hiyo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Geita, Bw. Thomas Dimme akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita (hawapo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma katika halmashauri hiyo.

Mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Bw. Evarist Kimori akiwasilisha hoja kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.

……………………………………….

Na. Veronica Mwafisi – Geita

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewaasa watumishi wa umma nchini katika maeneo yao ya kazi kuhakikisha wanalinda na kusimamia fedha zinazotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ili iwanufaishe Watanzania na taifa kwa ujumla.

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo, wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita akiwa kwenye ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma walio katika halmashauri hiyo.

Mhe. Ndejembi amewataka watumishi kutokuwa na tamaa ya kutumia fedha za miradi ya maendeleo kwa manufaa yao binafsi kwani kitendo hicho kinakwamisha jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuliletea taifa maendeleo.

“Tuache tabia ya kudokoa fedha za miradi ya maendeleo kwani jukumu la kulinda fedha hizo ni la watumishi wa umma wote si la viongozi pekee,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Akizungumzia kuhusu watumishi wa umma kutoa elimu juu ya jitihada za kuleta maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, Mhe. Ndejembi amewataka watumishi wa umma kutoa elimu kwa wananchi wanaowahudumia ili waelewe azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutafuta fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.

“Ni wajibu wetu kumsemea Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa yale mema ambayo analifanyia taifa kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo,”Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri wa Wilaya ya Geita Bw. Charles Kazungu ameishukuru Serikali kwa namna inavyowajali wananchi wa Geita kwa kuwapelekea fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameendelea na ziara yake ya kikazi Mkoani Geita kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments