UZALENDO NI TUNU KWA TAIFA: KATIBU MKUU MMUYA



Na Mwandishi wetu- Mara

Wasomi na vijana wamekumbushwa umuhimu wa kuwa wazalendo, kujenga ,kuiendeleza na kuilinda Nchi na watu wake kwaajili ya maslahi ya Maendeleo ya Taifa.


Akizungumza katika sherehe ya Mahafali ya 40 ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare kilichopo Wialaya ya Musoma Mkoani Mara Katibu Mkuu Mteule Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi  Bwa. Kaspar  Mmuya amesema mustakabali wa Maendeleo ya Taifa lolote Duniani unategemea mchango wa Taasisi za mafunzo katika kuandaa wataalam wenye weledi ambao ndio chachu ya kuleta mageuzi ya kifikra na maendeleo Jumuishi na endelevu kwa Jamii.


"Wizara inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Chuo hiki katika kuandaa wataalam wa fani ya maendeleo ya jamii ambao ndiyo injini ya kutafuta suluhisho la changamoto za maendeleo ya kijamii, kiuchumi, kiteknolojia, kiutamaduni, kisiasa na kimazingira kwa kutumia rasilimali zinazoizunguka jamii, hivyo mafunzo yanayotolewa hapa sharti yaakisi mipango ya nchi na vipaumbele vya jamii ili kuleta matokeo chanya ya maendeleo" Amesema Katibu Mkuu huyo.


Pia  Bwa. Mmuya amekipongeza Chuo hicho kwa kuanzisha programu ya uanagenzi ambayo imesisitizwa katika ilani ya Chama Cha Mapinduzi  (CCM) ya mwaka 2020/2025 ambapo hadi kufikia sasa baadhi ya wahitimu wa mafunzo ya uanagenzi wamepata ajira katika taasisi na makampuni mbalimbali Nchini.


Aidha Mmuya ametoa rai kwa Chuo kuhakikisha kinafanya utafiti kwa lengo la kuishauri serikali kuhusu changamoto zinazohitaji mabadiliko ya kisera ,kimkakati au kisheria.


"Kwa upande mwingine tafiti zinaweza kuwa na msaada mkubwa katika kubuni na kuboresha zana na mbinu shirikishi za kuhamasisha jamii kushiriki katika kubuni, kupanga, kutekeleza, kufuatilia na kutathimini shughuli au miradi ya maendeleo, hivyo jitahidini sana kutekeleza jukumu hilo kwa kiwango kikubwa",ameeleza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments