APIGWA SHOTI AKIWAHUJUMU TANESCO 'ALIKUWA ANAPIGISHA SHOTI UMEME UKATIKE"


Kigodi Juma, aliyepigwa shoti ya umeme

Kigodi Juma (24), mkazi wa Kijiji cha Nkiniziwa kilichopo wilaya ya Nzega mkoani Tabora, amejeruhiwa vibaya katika maeneo ya mwili wake baada ya kupigwa na shoti ya umeme wakati akikata nguzo ya umeme kwa kutumia shoka, majira ya usiku.


Akitoa ufafanuzi wa tukio hilo Afisa Mtendaji wa Kata ya Nkiniziwa Hamisi Bundu, amesema kijana huyo alitenda tukio hilo usiku wa kuamkia Oktoba 10, 2022 ambapo majira hayo ya usiku walishtushwa na kukatika kwa huduma ya umeme.

Amesema kijana huyo kabla ya kuanza kukata nguzo hiyo alirusha waya uliokuwa umefungwa vipande vya miti kwa ajili ya kupigisha shoti ili umeme uweze kukatika ili apate urahisi wa kuangusha nguzo hiyo bila wasiwasi wa kujeruhiwa na umeme pasipo kujua kama umeme bado ulikuwa haujakatika.

Kijana huyo baada ya kupigwa shoti ya umeme alikimbizwa katika kituo cha afya Busondo na kwa sasa anaendelea na matibabu, huku Kaimu Mganga wa kituo hicho cha afya Juma Sosoma, akieleza licha ahueni aliyonayo kwa sasa ataandikiwa rufaa ya kwenda katika hospitali kubwa kwa ajili ya vipimo zaidi vya ndani ya mwili kutokana na kuumia vibaya katika maeneo ya miguu,shingo ,usoni na kwenye mikono.

CHANZO- EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments