WAZIRI NAPE ATOA UFAFANUZI WA GHARAMA ZA BANDO....'PIA KUWENI MAKINI NA MATUMIZI YA SIMU JANJA'

 

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na taasisi za kimataifa, Tanzania inashika nafasi ya sita kwa Bara la Afrika kwa kuwa na gharama za chini za bando “vifurushi”  huku ikishika nafasi ya 32 Duniani kwa gharama ya chini ya data.

 

Waziri Nape ametoa ufafanuzi huo wakati aliposhiriki kipindi cha Power Breakfast on Saturday cha Clouds TV na redio, leo Agosti 20, 2022 jijini Dar es Salaam ambapo amesema bei ya data kwa wastani wa 1GB ni Dola 1.71 sawa na shilingi 3990.

 

“Tanzania kuwa miongoni mwa Mataifa yenye gharama za chini za mawasiliano haimaanishi kuwa itapunguza malalamiko kwa kuwa uchumi wetu haufanani na wananchi wengi wana kipato cha chini”, amesema Waziri huyo.

 

Amesema kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeendelea kufanya tathmini ya gharama za uwekezaji, utunzaji na usafirishaji wa data kila baada ya miaka minne na tathmini nyingine inafanyika mwaka huu ili kupata uhalisia wa gharama za bando kama zitapanda au kushuka.

 

“Wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa Serikali yao ni sikivu na inafanyia kazi malalamiko na maoni ya wananchi, lakini pia nitoe rai kwa wananchi kuwa makini na matumizi ya simu janja hasa kwenye kujiunga na huduma mbalimbali pamoja na programu tumizi “applications” ili kupunguza matumizi ya bando”, amesisitiza Waziri Nape.

 

Aidha, Waziri Nape amesema kuwa Serikali imeruhusu ushindani kwa kuweka mazingira wezeshi ya kuwa na kampuni nyingi zinazotoa huduma za mawasiliano ambapo huduma ya vifurushi ni huduma ya ziada inayotolewa na makampuni hayo na kuleta unafuu wa gharama za mawasiliano.

 

Ameongeza kuwa kwa ulimwengu wa sasa wa kidijiti huduma nyingi zinapatikana kwa njia ya mtandao, hivyo kuifanya huduma ya intaneti kuwa huduma muhimu na ya msingi katika kuendesha shughuli za uzalishaji na upatikanaji wa huduma za kijamii.

 

Katika hatua nyingine Waziri Nape ameielekeza TCRA, Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA- CCC) na Makampuni ya simu kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na kujibu au kutoa ufafanuzi wa maswali na malalamiko ya wananchi

 

Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments