TUME YA UTUMISHI WA WALIMU YATAJA MAKOSA VINARA KWA UTOVU WA NIDHAMU KWA WALIMU..YAMO MAPENZI


 Mwenyekiti wa TSC Profesa Willy Komba akiongea na waandishi wa habari Jijini Dodoma (hawapo pichani) kuhusu mwenendo wa maadili ya utumishi wa walimu nchini 

***

Na Dotto Kwilasa Malunde 1 blog, DODOMA.

TUME ya Utumishi wa Walimu Nchini (TSC) imetaja makosa  ambayo ni  vinara kwa utovu wa nidhamu yanayofanywa na walimu na kupelekea  kuchukuliwa hatua za kinidhamu katika kipindi cha mwaka 2020/21 ambapo jumla ya walimu 1795 walichukuliwa hatua kutokana na makosa hayo.


Mwenyekiti wa TSC Profesa Willy Komba amesema hayo leo Disemba 29,2021 katika Mkutano wake na waandishi wa  habari ambapo ametaja makosa hayo kuwa ni pamoja na utoro huku akibainisha kuwa jumla ya walimu 931 walishtakiwa, kugushi vyeti walimu 461, uhusiano wa mapenzi na wanafunzi walimu 211, ukaidi asilimia 6.3 na ulevi makosa 184 sawa na asilimia 4.5 ya makosa yote.


Amesema licha ya changamoto hizo bado kuna walimu waadilifu ambao wanaendelea kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kupandisha viwango vya ufaulu katika shule za msingi na sekondari .

Kuhusu vitendo vya utovu wa nidhamu mwenyekiti huyo ametaja vitendo vya utovu wa nidhamu ambavyo vimekuwa vinara kwa sekta hiyo katika kipindi Cha mwaka Januari 2020/21 na Julai/ Desemba 2021.


"Walimu wengi bado watoro , hivyo sisi kama  TSC katika kipindi hicho tumewachukulia hatua za kinidhamu,lakini pia tunawakumbusha walimu kurudi kwenye misingi ya maadili ya utumishi wa umma, jumla ya walimu 1795 walichukuliwa hatua ikiwemo utoro ambapo walimu 931 walistakiwa, kugushi vyeti walimu 461, uhusiano wa mapenzi walimu 211, ukaidi Asilimia 6.3 na ulevi Asilimia 4.5 ya makosa yote", amesema.


Amesema katika vitendo hivyo suala la utoro wa walimu ndilo lililoongoza ambapo walimu 931 walistakiwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali katika kipindi cha Januari/Juni sawa na asilimia 51.9 ya makosa yote huku kipindi cha Julai/Septemba mwaka huu makosa hayo yalikuwa 105 na kuchukuliwa hatua mbalimbali.


KUGUSHI VYETI

Profesa. Komba ametaja kosa ambalo linashika nafasi ya pili kuwa ni vitendo vya kugushi vyeti vinavyofanywa na baadhi ya walimu ambapo walimu 461 walistakiwa sawa na asilimia 25.7 katika kipindi cha Januari/Juni 2021 na kesi 41 katika kipindi cha Julai/Septemba 2021.


UHUSIANO WA MAPENZI  WA WALIMU NA WANAFUNZI

Amesema kosa hilo linashika nafasi ya tatu kwa utovu wa nidhamu ambapo katika kipindi cha januari/Juni jumla ya walimu 211 walistakiwa sawa na asilimia 21.8 huku katika kipindi cha Julai/Septemba kikiwa na kesi 31 sawa na asilimia 16.8 ziliripotiwa.

Pamoja na hayo ametumia nafasi hiyo kuwaasa walimu nchini kuwapa uhuru wanafunzi ikiwa ni pamoja na kuwaheshimu ili wasome vizuri.


Amesema ni wajibu wa Mwalimu kumlea mtoto kimwili na kiroho ikiwemo kumkinga na madhara ya ubakaji,madawa ya kulevya na mengineyo.


"Tunaposikia Mwalimu amejihusisha na mapenzi na wanafunzi anakuwa amekiuka yote hayo,wajibu mwingine wa Mwalimu ni kumlea kiroho mtoto anawajibika kumlea kwa kuwa anatumia muda mwingi shuleni kuliko nyumbani,"amesema.


VITENDO VYA UKAIDI 

Kuhusu vitendo vya ukaidi ametaja kosa hilo kushika nafasi ya nne ambapo makosa yaliyoripotiwa yalikuwa asilimia 6.3 katika kipindi cha Januari/Juni na katika kipindi cha Julai/Septemba  mwaka huu ni asilimia 1.6.


"Mwalimu anapaswa kumuelimisha mwanafunzi aheshimu watu wa rika zote kwa kuzingatia kuomba msamaha anapokosea,awe na hofu ya Mungu ndiyo maana tuna vipindi vya dini,ukaidi unayofanywa na baadhi ya walimu unawaharibu watoto wanabaki na viburi ,lazima walimu muwasimamie watoto  kupendana na kuwa na utayari wa kusaidiana,"ameeleza.


Mbali na hayo ameeleza kuwa masuala ya nidhamu wasiachiwe viongozi wa dini   peke yao bali walimu pia wana jukumu la kutunza fikra na mahusiano ya mwanafunzi ili kuwalea vizuri ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kila somo lazima walimu wahakikishe linamjenga mwanafunzi kiakili, kiutendaji , kiroho na kijamii.


WALIOPEWA ADHABU

Alisema kutokana na makosa hayo zipo hatua mbalimbali ambazo zilichukuliwa dhidi ya wahusika kulingana na makosa yao asilimia 57.1  walifukuzwa kazi katika kipindi hicho cha mwaka Januari/Juni 2020/21, Julai/Septemba 46.7 huku waliopewa kalipio ni asilimia 8.5 kipindi cha Januari/Juni ilikuwa asilimia 8.5 huku Julai/Septemba ikiwa ni asilimia 7.1.


Profesa. Komba amefafanua kuwa asilimia 8.5 walishushwa daraja katika kipindi cha Januari/Juni na Julai/Septemba walioshushwa vyeo 7.6,walioshushwa mshahara walikuwa asilimia 7.7 katika kipindi cha Januari/Juni na kipindi cha Julai/Septemba 9.8, walipewa onyo katika kipindi cha Januari/Juni 7.2 na Julai/Septemba walikuwa asilimia 16.8.


"Katika kipindi hicho wapo watumishi walioshtakiwa na baada ya kutathimini mashauri yao kwa kuzingatia kanuni, Sheria na taratibu waligundua kuwa hawakuwa na hatua ambapo walikuwa asilimia 5.5 Januari/Juni na asilimia 10.5 kipindi Julai/Septemba",ameeleza.


"Adhabu zinazotolewa zinalingana na kanuni na taratibu za tume ya Utumishi  ila kwa wale ambao hawaafiki na maamuzi ya viongozi wanakata rufaa kwa mamalaka ya nidhamu  ngazi ya Wilaya, baadaye kwa TSC na mwisho kabisa wanakata rufaa kwa Rais,"amesema.


Kutokana na hayo, mwenyekiti huyo ametoa wito kwa walimu kuhakikisha wanaijua TSC ,wajibu wao ,kanuni na taratibu zinazosimamia utumishi wao ikiwa ni pamoja na  kuzingatia maadili na kuwatendea haki wanafunzi na kuzingatia maagizo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Ummy Mwalimu ya kuwataka kuwaacha watoto wapumzike kipindi cha likizo.

Katika hatua nyingine amemshukuru na kuipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kuufanya mwaka 2021 kuwa mwaka wa baraka kwa sekta ya elimu nchini kwa kufanikisha kupandisha madaraja na kulipa mishahara mipya baada ya kupandishwa ambapo takribani walimu 146000 walipandishwa vyeo.


Amesema,tangu Rais Samia aingie  madarakani umekuwa mwaka wa neema kwa sekta ya elimu nchini tofauti na vipindi vingine vilivyopita.


"Katika kipindi cha mwaka mwaka huu wameweza kupandisha madaraja na kuanza kulipa viwango vipya vya mishahara jambo ambalo huko nyuma halikuweza kufanikiwa ,tume  inampongeza Rais Samia na Serikali yake kwa kuendelea na juhudi za kuboresha miundombinu ya elimu hapa nchini hususani kupitia fedha ya UVIKO-19 iliyotolewa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya ujenzi wa madarasa,"amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments