GGML, RAFIKI SURGICAL MISSION WATOA GARI LA WAGONJWA KWA ZAHANATI BUKOLI – GEITA


Makamu Rais wa GGML, Simon Shayo (kulia) akimkabidhi kadi ya gari Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Geita, Ali Kidakwa (kushoto.) 
Makamu Rais wa GGML, Simon Shayo (kulia) akisalimiana na baadhi ya wafanyakazi wa Kituo cha Afya Bukoli- Geita katika hafla ya kukabidhi gari la kubeba wagonjwa. 
****
NA MWANDISHI WETU, GEITA 
Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na Rafiki Surgical Mission kutoka Australia wametoa msaada wa gari la wagonjwa lenye gharama ya Sh milioni 32 kuhudumia wagonjwa katika kituo cha Afya cha Bukoli na maeneo jirani wilayani Geita. 

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya gari hilo katika Kituo cha Bukoli Wilayani Geita, Makamu Rais anayeshughulikia Mahusiano na Maendeleo endelevu, Simon Shayo amesema msaada wa gari hilo umetolewa kwa wakati na utasaidia kutatua changamoto za usafiri kwa wagonjwa mahututi katika kata hiyo ya Bukoli na maeneo ya jirani. 

“Halmashauri ya Wilaya ya Geita iliomba msaada wa gari la wagonjwa kutoka GGML ili kuwasaidia wagonjwa katika jamii ya watu wa Bukoli ambao waliokuwa na changamoto kubwa kila ilipobidi kusafirisha wagonjwa kwa ajili matibabu makubwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Geita ambayo ipo wastani wa kilomita 35 kutoka kijiji cha Bukoli. 

" Ushirikiano kati yetu na Rafiki Surgical Mission ni mwitiko wa maombi hayo na umekuja muda mwafaka kwa kuwa wamekuwa pia na dhamira ya kusaidia huduma za afya mkoani Geita kwa miaka kadhaa sasa,” alisema Bw Shayo. 

Kwa karibu miaka 20 sasa, mbali na kutoa msaada wa vifaa tiba, Geita Gold Mining Limited kwa kushirikiana na Rafiki Surgical Mission wameongeza wigo wa matibabu kwa watoto na watu wazima mkoani Geita ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya midomo sungura na migongo wazi kwa kuwapatia matibabu ya upasuaji bure. 

Bw Shayo amefafanua kuwa GGML pia walitoa msaada katika kituo cha afya cha Bukoli mwaka 2004 kwa kujenga jengo la Wagonjwa wa Nje (Outpatient Department) na nyumba ya watoa huduma wa afya. GGML pia imefadhili miradi mbalimbali ya afya wilayani Geita ikiwemo ukarabati wa Hospitali ya Rufaa mkoani Geita na ujenzi wa vituo vipya vya afya katika vijiji vya Nyamalembo, Nyakahongola, Kasota na Kakubiro ambapo miradi yote hiyo kwa pamoja iligharimu Shilingi bilioni moja na milioni mia nane (1.8bn) za Kitanzania. 

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ali Kidwaka kwa niaba ya Serikali ametambua mchango wa GGML katika kutatua changamoto ya huduma za afya katika halmashauri ya wilaya na kwengineko mkoani Geita na kuwaomba washirika wengine waliopo katika Wilaya ya Geita kushirikiana na Serikali kwa lengo hilo hilo. Aidha mwaka 2019, GGML ilichangia pia vifaa tiba vyenye gharama ya Shilingi za kitanzania milioni 142 katika vituo vya afya vya Katoro na Bukoli. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم