WAZIRI SIMBACHAWENE APIGA MARUFUKU POLISI KUKAMATA WANANCHI, BODABODA BILA KUFUATA UTARATIBU

Na Mwandishi Wetu, MOHA, Mpwapwa.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amepiga marufuku ukamataji wa wananchi, bodaboda pamoja na kufanya operesheni ya aina yoyote kwa kukurupuka bila kufuata utaratibu, hali inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani badala ya kujenga amani.

Pia Waziri huyo aliagiza kuwa, kila operesheni itakayopangwa kufanywa na Polisi Nchini, wanapaswa watoe taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ili ajue nini kitafanyika kwa kuwa yeye ni Mwenyikiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, na pia ndio utaratibu unapaswa kuwa hivyo.

Akizungumza katika Kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama cha Wilaya ya Mpwapwa, Mkoani Dodoma na baadaye kulisisitiza agizo hilo katika Kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya, leo, Simbachawene alisema ukamataji usio na mpangilio hauna tija na unaweza kuvunja amani badala ya kujenga amani.

“Wananchi wanawalalamikia askari wetu sana kukamata bodaboda bila sababu, sio bodaboda tu hata kukamata kamata hovyo watu, ukamataji mwingine unakua kama kukomoana, hauna tija, hauleti amani, badala yake unasababisha amani itoweke,” alisema Simbachawene.

Aliongeza kuwa, “Yaani msako fulani unatungwa hauna kichwa wala mguu, hauna maelekezo yoyote ya Mkuu wa Jeshi la Polisi au chombo, ni watu tu wanajitungia wanaondoka na pikipiki yao wamepakiana wanaenda kufanya operesheni ambayo haina utaratibu.”

Alisema vyombo vya ulinzi na usalama ni vya wananchi, na operesheni yoyote haipaswi kufanyika bila Mkuu wa Wilaya kupewa taarifa ambapo ndio utaratibu unapaswa kuwa hivyo.

Pia Waziri Simbachawene aliupongeza uongozi wa Wilaya hiyo kwa kuwa karibu na wananchi kwa kusikiliza kero zao na kuifanya Wilaya hiyo kuendelea kuwa na amani na utulivu na wananchi kuendelea kuwa na imani na viongozi hao.

“Endeleeni kuwa karibu na wananchi, kwa kusikiliza kero zao na pia kuzitatua, na epukeni malalamiko ya hapa na pale yasiyokuwa ya lazima,” alisema Simbachawene.

Aidha, Simbachawene aliewaomba viongozi wa Wilaya hiyo kujipanga vizuri katika maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

“Mwaka huu ni wa uchaguzi, wananchi kupitia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama na taasisi zote za utawala, mnapaswa kuwa na ushirikiano mkubwa ili kujenga msingi wa uchaguzi utakaokuwa wa amani na utulivu,” alisema Simbachawene.

Alisema mwaka wa uchaguzi haupaswi kuwa na vurugu, ni mwaka ambao unapaswa kuwa na utulivu kwasababu ni jambo zuri la kidemokrasia linafanyika.

“Rai yangu kwa wananchi, kuhakikisha kwamba tunapaswa kujenga utulivu kuanzia sasa kuelekea uchaguzi mkuu, hatupaswi kuwa na vurugu, ni mwaka ambao amani na utulivu wa nchi unajengwa kuanzia sasa, mshikamano wa vyombo vyetu ndio msingi wa kujenga uchaguzi utakao kuwa wa huru na haki ambao utafanya mwaka huu,” alisema Simbachawene. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Jabir Shekimweri alimshukuru Waziri huyo na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yake aliyoyatoa katika kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Kikao cha Baraza la Madiwani.

Naye Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mpwapwa (OCD), ASP Maulidi Manu alisema ujio wa Waziri huyo umewasaidia zaidi kwa kujipanga zaidi, na kufuata maagizo yote aliyoyatoa kwa Jeshi la Polisi Wilayani humo.

“Tumefarijika kwa ujio wa Mheshimiwa Waziri, maagizo yake aliyoyatoa tunaahidi kuyafanyia kazi,” alisema Manu.

Waziri Simbachawene, alifanya ziara ya siku moja kwa ajili ya kukutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Baraza la Madiwani Wilayani humo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527