MAJUKWAA YA HAKI JINAI YA MIKOA YOTE YAZINDULIWA KITAIFA SINGIDA


 Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi aliyesimama akizindua Jukwaa la Haki Jinai Mkoa wa Singida. Kushoto ni Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP) Nchini, Biswalo Mganga na kulia in Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angerina Lutambi
 Picha ya pamoja  baina ya Mkrugenzi wa Mashitaka,(DPP) Biswalo Mganga mwenye suti , Mkuu wa Mkoa wa Singida (mwwnye kilemba) anayefuata Dkt.Angelina Lutambi  Katibu Tawala Mkoa wa Singida na wajumbe wa Jukwaa la Haki Jinai Mkoa wa Singida Mara baada ya kuzinduliwa kwa Jukwaa hilo la Mkoa
Baadhi ya  watumishi wa Umma Singida walioshiriki kwenye uzinduzi wa Jukwaa la Haki Jinai Mkoa wa Singida( Picha Zote na John Mapepele,Singida


Na John Mapepele, Singida


Mkuu wa Mkoa wa Singida,  Dkt. Rehema Nchimbi amezindua Jukwaa  la Mkoa  la Haki  Jinai leo huku  Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Nchini,  Biswalo Mganga  akisema kuwa  uzinduzi huu unafanywa  kitaifa mkoani Singida  na kuelekeza  mikoa yote nchini kuzindua ili kusaidia  kupambana   na uhalifu wa kijina katika  mikoa husika hivyo kupunguza mrundikano wa  mahabusu.



Dkt. Nchimbi amesema kuzinduliwa kwa Jukwaa hili kutakuwa nguzo kuu ya kuzima uhalifu katika Mkoa wa Singida, huku akiwataka wajumbe kutumia jukwaa hili  kufanya utatifi na kutafakari kwa kina  ni  namna  gani bora ya kudhibiti uhalifu  badala  ya kusubili  utokee na kupeleka kesi mahakamani, jambo ambalo amesema  madhara yake yamekuwa  makubwa.


“Namshukuru Mungu. Leo, kwangu ni siku ya kihistoria na ya kipekee ambayo  nilitamani  kuona inatimia  tangu siku nyingi. Kila wakati nimekuwa nikiwasisitiza  kuwa ni muhimu na ni lazima vyombo vyote vya Serikali katika mkoa wetu kufanya kazi ya kupambana  na uhalifu kwa  pamoja  badala ya kila  mmoja kujiona  ni bora zaidi katika  nafasi yake jambo halina tija  na halitusaidii kama taifa, lakini hatimaye leo hili linatimia” alisisitiza



Aidha amewataka Wajumbe kufanya kazi  kwa umoja  na uzalendo  ili jukwaa hilo liwe mfano  bora na mikoa mingine  waje kujifunza.


“Kama  kwenye  mambo mengine tumeweza  kushika nafasi za kwanza  kitaifa kwa nini  tusiwe wa kwanza  katika  kufanya kazi  nzuri kwenye  kutekeleza majukumu ya jukwaa la Haki Jinai kwenye Mkoa wetu na wengine waje kujifunza kwetu, inawezekana endapo kila mtu atatekeleza wajibu wake” alisisitiza  Dkt. Nchimbi


Dkt. Nchimbi  amesema  hata vitabu vitakatifu  vimeandika  mwisho ya  uhalifu ni mbaya  na kwamba  msharaha wa dhambi  ni mauti na kuelekeza kuwa kila  Ofisi  na Idara ya Serikali  katika Mkoa wa Singida kuwa  na mfumo wa  Jukwaa la Haki Jinai ambao utasaidia kujenga  mfumo wa kutafakari na kudhibiti uhalifu badala ya kusubiri utokee.


Amesema ili kuwa na ufanisi na tija  wa kutokomeza uhalifu kwenye Mkoa wake ameyataka  majukwaa ya Haki Jinai ya kila Wilaya  kuanza mara moja  kufanya kazi na kupeleka mapendezo  yake  katika Jukwaa la Mkoa  kwa  kuwa  Jukwaa la Mkoa linategemea  utendaji wa  majukwaa ya Wilaya.


Akizungumza katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida kabla  ya uzinduzi huo , Mganga amesema kwa  mujibu wa Sheria ya Mashitaka  na 27 ya mwaka 2008 ibara  ya 59(B) (II) na  kwa mujibu wa Katiba ya Nchi, Mkurugenzi wa Mashitaka ndiye mwenye jukumu la kuratibu upepelezi  wa kesi zote za jinai nchini japokuwa anaweza  kukasimu madaraka hayo kwa vyombo  vingine vya Serikali.


Amesema Ofisi  yake imedhamilia  kutokomeza uhalifu wa kijinai kwa  kutekeleza mkakati wa kuunda kwa  majukwaa  ya Haki Jinai kila  Mkoa hapa nchini  ambalo  ni takwa la kisheria  ili kuwa  muarobani wa kuthibiti   matukio na kesi za kijinai badala  ya kusubiri  makosa yafanyike na kutoa hukumu jambo ambalo amesema  halina tija  kwa  wananchi na taifa kwa ujumla.


Mganga amesema  kwa  kuzingatia  ukubwa wa  tatizo   na ongezeko wa uhalifu wa kijinai Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais, John Pombe Joseph Magufuli iliamua  kufanya marekebisho  makubwa ya kupambana na tatizo hili ambapo iliunda  Ofisi ya Taifa  ya Mashitaka  kwa kutangaza  kwenye  gazeti la Serikali namba 49,  tarehe 13/2/2018 tofauti na awali ambapo  Kurugenzi ya  Mashitaka (DPP) ilikuwa chini  ya Ofisi ya Mwanasherioa Mkuu wa Serikali.


Amewataka  wajumbe wote wanaounda  jukwaa  hilo  kufanya kazi kwa weredi na kushirikiana  ili kuhakikisha mazingira ya  shughuli za kijinai yanakwenda vizuri ambapo amesema majukwaa  ya Mkoa yanatakiwa  kutoa mapendekezo ya  nini kifanyike  kwenye Jukwaa la Haki Jinai la Taifa kwa ajili ya utekelezaji na ufuatiliaji.


Amesema kuliungana na Sheria ya Mashitaka, Jukwaa la Haki Jinai la Mkoa linatakiwa kukaa vikao visivyopungua  viwili kwa  mwaka  ambapo amesisitiza   wajumbe kuhudhuria wao wenyewe badala ya kuja wawakilishi kwa kuwa  sheria inawataka wajumbe halisi na sio wawakilishi na kuongeza kuwa  kama kunakuwa na ulazima  au umuhimu, vikao hivyo  ninaweza  kuketi zaidi ya mara mbili kwa  mwaka kadri ya mahitaji.


Mkurugenzi, Mganga ameelekeza  Jukwaa la Haki Jinai Mkoa wa Singida  kuanza kazi mara mmoja  ili kutatua  changamoto mbalimbali zinazokabili  uhalifu katika mkoa ambapo amelitaka  kuketi  mara mbili kabla ya Oktoba mwaka


Mwenyekiti wa Jukwaa la Mkoa wa Singida, Rose Chilongozi  ambaye ni Mwendesha Mashitaka Mkoa wa Singida alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Singida   kwa kuzindua Jukwaa hilo na  kumhakikishia kuwa yeye na wajumbe wake watafanya kazi kwa ushirikiano  mkubwa ili  kudhibiti uhalifu katika  mkoa huo.


 Katibu wa Jukwaa la Haki Jinai Mkoa wa Singida ambaye  ni  Mkuu wa Upelelezi Mkoa huo, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Stela  Mutabihirwa amewataja  wajumbe wa  Jukwaa hilo kuwa ni pamoja na Mwendesha Mashitaka wa Mkoa ambaye ni Mwenyekiti, Mkuu wa upelelezi wa Mkoa ambaye ni Katibu, Mkuu wa Usalama wa Taifa wa Mkoa, 

Wengine ni Afisa Ustawi wa Mkoa, Mwenyekiti wa  Bodi ya Parole  wa Mkoa, Afisa Mkemia Mkuu wa Mkoa,  Afisa-Bwana Huruma wa Mkoa, Mwanasheria kutoka Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa na Afisa  wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa  na mdau mwingine yoyote ambaye wataona anafaa  kumwalika  kushughulikia jambo husika.


Kamishina  Msaidizi wa Polisi Mutabihirwa  ambaye  ni Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Singida amesema  kwa upande wa Polisi anaishukuru Serikali kwa kuharakisha kuzindua  jukwaa hilo kwenye Mkoa wa Singida kwa kuwa litasaidia  kutatua changamoto mbalimbali za uhalifu.


“Napenda kumshukuru Mheshimiwa, Rais Magufuli kwa  kuunda  chombo  hiki kupitia Ofisi  ya Mashitaka  kwani kwa sisi Jeshi la Polisi tutashikisha dawati letu la  Polisi Jamii ambapo sasa  naamini  tutatoa elimu mashuleni na kupunguza mimba za utotoni pia uhalifu wa mauaji,  ukatili wa kijinsia na migogoro ya ardhi na mashamba  ya wananchi katika Mkoa wetu itapata  ufumbuzi wa kudumu” ameongeza  Afande Mutabihirwa  


Akifungua rasmi kikao cha uzinduzi wa Jukwaa hilo Katibu  Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi amesema  kila mwananchi anawajibu wa  uzuia uhalifu  ili Mkoa wa Singida uwe sehemu salama.


Aidha aliwaasa wajumbe  kufanya  kazi kwa kuzingatia sheria  ili kuwa ukuta imara wakuzuia aina yoyote ya uhalifu ambao unaweza kupenya  na kuingia makao makuu ya nchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم