POLISI DODOMA WAKANUSHA MTOTO WA MTOTO KUFUNGIWA KABATINI

Wakati binti wa kazi akieleza jinsi mwanaye mwenye umri wa miezi mitano alivyofungiwa kabatini na mwajiri wake mkoani Dodoma kwa muda wa miezi sita, Jeshi la Polisi mkoani humo limekanusha madai ya mtoto huyo kufungiwa kabatini.

Binti huyo wa miaka 15, jana Desemba 30, 2018 akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma alidai kufanyiwa ukatili kwa kupigwa na kufanyishwa kazi hadi usiku wa manane na bosi wake anayedaiwa kuwa ni mwalimu na kwamba amekuwa akimwambia amfungie hadi usiku mtoto wake na kila alipovunja masharti alikumbana na kipigo.

Leo Desemba 31, 2018 polisi mkoani Dodoma imekanusha madai ya mtoto huyo kufungiwa kabatini kama inavyodaiwa, lakini wamekiri binti huyo kushambuliwa na mwajiri wake.

Kamanda wa polisi mkoani humo, Gilles Muroto amesema polisi wamefanya upekuzi katika nyumba ya mwajiri wa binti huyo ambaye kitaaluma ni mwalimu, Anitha Kimako na kubaini hakuwa na kabati nyumbani kwake.

"Kesi ya shambulio ipo na ameshambuliwa kweli na ndiyo maana tunamshikilia. Anashikiliwa kutokana na usalama wake kwani kelele za watu ni nyingi, ila hili suala la kuwekwa mtoto kabatini halipo," amesema Muroto.

Amesema uchunguzi wa kina unafanyika na kwamba lazima mwalimu huyo wa Shule ya Msingi Medali afikishwe mahakamani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527