ALIYEPIGWA RISASI NA POLISI DAR AFARIKI


MKAZI wa Mbagala Charambe wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam, Linus Nyoni(42) amefariki dunia baada ya kujeruhiwa na risasi wakati akijaribu kuwakimbia askari polisi baada ya kukamatwa akituhumiwa kwa uhalifu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema walipata taarifa kwamba kuna mtu anafanya matukio mbalimbali ya uhalifu wa kutumia silaha katika maeneo ya Mbagala Kibondemaji.

“Baada ya taarifa hizo tuliweka mtego wa kumkamata mtuhumiwa huyo ambaye ni Nyoni na baada ya kumpekua alikutwa na bastola ndogo aina ya revolver ikiwa na risasi sita ndani ya magazine huku namba za bastola hiyo zikiwa zimefutwa,” amesema Kamanda Mambosasa.

Alisema mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na matukio mbalimbali ya unyang’anyi wa kutumia silaha maeneo ya Mbagala na Mkuranga huku akishirikiana na wenzake huku akisema wana silaha zingine walizoficha kwenye Msitu wa Dona na maeneo ya Buza na kukubali kuwapeleka kuwaonesha wenzake walipo.

“Polisi waliongozana na mtuhumiwa huyo mpaka Msitu wa Dona na walipofika mtuhumiwa huyo alikimbia huku akipiga makelele kuwashtua wenzake na ndipo askari walifyatua risasi hewani na kumuamuru asimame, lakini hakutii amri hiyo, ndipo askari wakafyatua risasi nyingine zilizomjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake,” alisema.

Hata hivyo, alisema mtuhumiwa huyo alichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu na mwili wake umehifadhiwa ukisubiri utambuzi.

Amesema polisi linaendelea na msako mkali wa kuwatafuta wenzake aliokuwa akishirikiana nao pamoja na silaha wanazotumia katika uhalifu.

Katika tukio lingine, polisi inamshikilia Majid Abdallah (31), mkazi wa Tabata wilayani Ilala kwa kukutwa na magazine moja na risasi 35 za bastola ndogo aina ya browing akiwa amezificha chini ya uvungu wa kitanda chake katika chumba anachoishi.
Chanzo- Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527