MPAMBE WA LOWASSA APIGWA RISASI,LOWASSA ADAI WAHUSIKA NI MAJAMBAZIMjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya Arumeru na Diwani wa kata ya Mlangarini wilayani humo, Mathias Manga, amenusurika kuuawa baada ya watu wasiojulikana waliokuwa wakimfuatilia kumpiga risasi nje ya geti la nyumba yake.

Tukio hilo lilitokea saa 4:45 usiku wa kuamkia jana.

Manga ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu wa Tanzanite huko Mirerani, mkoani Arusha ni mmoja kati ya marafiki wakubwa wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye ametangaza nia ya kuomba ridhaa ya CCM kumteua kuwa mgombea wa kiti cha urais katika uchaguzi mkuu mwaka huu.

Manga alikuwa Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya kumtafutia wadhamini Lowassa mkoani Arusha, kazi ambayo ilikamilika jana baada ya kupata wadhamini 12o,339.

Haijafahamika rasmi iwapo tukio la kupigwa risasi na kujeruhiwa kwake, lina uhusiano wowote wa kibiashara au kisiasa, kwa sababu Manga mwenyewe hakutaka kuzungumza na waandishi wa habari kuhusiana na suala hilo.

Hata hivyo, akizungumza kwa njia ya simu na waandishi wa habari jana, Manga alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Awali alisema angezungumza na waandishi wa habari baada ya nusu saa kwa vile alikuwa katika mazingira ambayo hayakuwa mazuri kuzungumza, lakini alipopigiwa tena simu alisema hawezi kuzungumza chochote.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo eneo la Ngarenaro.

Alisema risasi hiyo ilimparaza Manga maeneo ya ubavu wa kulia.

“Alitoka katika shughuli zake za kawaida na alipokuwa anarejea nyumbani kwake eneo la Ngarenaro kwenye nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa, ghafla aliona gari likimfuata kwa nyuma na alipokuwa akitembea kwa kasi nalo liliongeza mwendo, akahisi watu hao wanamfuata, hivyo akazidi kuongeza mwendo hadi alipofika getini kwake na lile gari pia lilieggeshwa kwa nyuma yake," alisema.

Alifafanua kuwa baada ya kuegesha gari hilo, kati ya wale mmoja wao alishuka akiwa ameshika kisu na mwingine bunduki.

Kamanda Sabas aliongeza kuwa baada ya Manga kuona hivyo, naye alitoa bastola yake kwa lengo la kujihami.

"Manga alipotoa silaha yake ili kujilinda, alishtukia akipigwa risasi lakini kwa bahati nzuri haikumpata vizuri…ilimpata maeneo ya nyama kwenye mbavu upande wa kulia na watu hao wakakimbia.”

Alisema kwa maelezo ya Manga watu hao walikuwa watano na wote walikimbia bila kuchukua kitu chochote na yeye alipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru kwa matibabu ambako alipata matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani kutokana na kutoumia sana.

Kamanda Sabas aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linawatafuta wahusika wa tukio hilo kwa njia zote ili wakipatikana wachukuliwe hatua za kisheria.

LOWASSA ASIKITIKA ATOA POLE
Lowassa jana wakati wa kudhaminiwa mkoani Arusha jana, alimpa pole Manga kutokana na tukio hilo kinalidaiwa kufanywa na majambazi.

Lowassa alisema anashukuru Mungu kwa kumnusuru na kusema kwamba anamtakia afya njema ili aendelee na kazi zake.

ASEMA HATISHWI
Wakati huo huo, Lowassa amesema hatishwi na vitendo vya kejeli, matusi yanayotolewa dhidi yake na havitamkatisha tamaa katika safari yake ya matumaini na kusisitiza anatosha kuwa Rais.

Lowassa aliwasili jana jiji hapa akitokea Dodoma.

Baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa ya Kilimanjaro (KIA), alianza safari yake kwa magari kuelekea Arusha kusaka wadhamini.

Akiwa njiani msafara wake ulizuiwa na wananchi mara zaidi ya mara tatu wakati akielekea katika Chuo cha Biblia cha Sakila cha kanisa la International Evangelism Church wilayani Arumeru ambapo alialikwa kwaajili ya kuombewa.

Akitoa neno la shukurani katika kanisa hilo, Lowassa alisema waendelee kupiga magoti na kumuombea ili aweze kufanikiwa katika safari yake ya matumaini kwani safari hiyo ina milima na mabonde.

Alisema kumekuwapo na maneno ya kejeli yanayotolewa dhidi yake na matusi lakini hata kata tamaa kwani yeye binafsi anaona anafaa kuwa Rais kuwatumikia watanzania.

“Nipo katika harakati za kutafuta wadhamini ambao hawapatikani kanisani wanapatikana mtaani ambako ndiko CCM ilipo, la kwanza naomba mniombee nayaweza yote kwa yeye anitiae nguvu, naomba mpige magoti msali sana,” alisema Lowassa.

Akizungumza katika Ibada ya maombezi, Askofu wa kanisa hilo, Dk. Eliudi Isanja, alisema anajua Lowassa anagombea urais na wanamuombea katika safari yake ambayo anaamini watanzania wengi wanaungana nayo.

Awali katika neno lake la shukurani alianza kwa kumpa pole Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM (NEC) wilaya ya Arumeru Mathias Manga, ambaye alivamiwa na majambazi wakampiga risasi lakini anashukuru hali yake inaendelea vizuri.

“Mungu ni mwema sana lakini kwa bahati nzuri haijaingia mwilini, tunaendelee kumuombea Afya yake iendelee vizuri ili afanye shughuli zake kwa amani,” alisema Lowassa.

Akitangaza waliojitokeza kumdhamini Katika Mkoa wa Arusha,Katibu Mwenezi wa CCM Mkoani humo, Issac Joseph, alisema Lowassa amedhaminiwa na wanachama wa CCM 120,336 kati ya wanachama hai 198,795.

Akiwashukuru wanachama waliojitokeza kumdhamini, Lowassa alisema anawashukuru waliomdhamini na imani yao kwake ataijibu kwa vitendo.

Alisema haiendi Ikulu kung’aa macho bali anaenda kuhakikisha kupambana na umasikini na atafanya maamuzi magumu kuhakikisha aleta ajira kwa wingi nchini na viwanda kwa wingi ili ajira zapatikane na watu waondokane na umaskini.Imeandikwa na Cynthia Mwilolezi, John Ngunge na Agusta Njoji, Arusha -NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم