Bibi kizee anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka
(70), asiyejulikana jina wala makazi yake,ameanguka akiwa uchi wa mnyama kisha
kuanza kutembea kwa kutumia makalio nyumbani kwa Suzana Mwandu mkazi wa mtaa wa
Mageuzi manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga, wakati akiwa katika
safari zake kwa kile kinachodaiwa kuwa ni imani za kishirikana.
Akielezea tukio hilo juzi mama mwenye nyumba
alikonasa kikongwe huyo bibi Mwandu alisema majira ya saa moja asubuhi
Januari 29 mwaka huu, alipoamka kuwaamusha wajukuu zake waende shule, ndipo
alipomkuta kikongwe akiwa amelala uchi wa mnyama nje ya nyumba
yake.
Bi Mwandu alisema, baada ya kikongwe huyo
kuanguka alijivuta ndani ya jiko lake lililoko nje ya nyumba ambalo lipo wazi,
na baada ya kuanza kumsemesha ndipo kikongwe akazinduka na kuanza kuongea
maneno ya ushirikina, hali ambayo ilimtia wasiwasi na kutoa taarifa kwa uongozi
wa serikali ya mtaa.
“Nyumba yangu nimeizindika vilivyo, hivyo
kikongwe huyu alipokuwa katika safari zake na kupita maeneo ya nyumbani kwangu
ndipo akakutana na balaa hilo na hatimaye akajikuta ameanguka na kujivutia
ndani ya jiko kwa ajiri ya kujistiri” alisema Bi Mwandu.
“Unajua siku zote mchawi anapoanguka na
ukimwacha kwa muda mrefu bila ya kumsemesha, anaweza kupoteza maisha, hivyo
kutokana na mimi kutokuwa na ubaya naye nikaona bora nimusemeshe, ili kumuokoa,
na baada ya hapo nikampa nguo za kujistili na aibu ya kuwa
mtupu”,aliongeza Bi Mwandu.
Kwa upande wao mashuhuda wa tukio hilo waliiambia malunde1 blog kuwa bibi huyo huenda akawa ni mchawi kutokana na kauli zake tatanishi na maneno ya kichawi
aliyokuwa anayatamka huku mikono yake ikionekana kukatwa kwa mapanga na kuota
sugu.
Walisema kikongwe huyo alikuwa haongei na
alikuwa hawezi kusimama na badala yake alikuwa anatembelea makalio yake
kutokana na kukosa nguvu.
“Huyu bibi atakuwa mchawi angalia hata mikono
yake imekatwa katwa na imekomaa kweli huenda huwa anajigeuza fisi na kutembelea
mikono,halafu macho yake siyo ya kawaida,ana kiburi kupita kiasi na ndiyo tabia
za wachawi wengi”,alieleza Halima Juma.
“Bibi huyu kafanya vituko,katoa pesa shilingi
hamsini,mia mbili,mia tano na elfu moja kutoka kiunoni mwake akaanza kuzirusha
na ndipo kapata nguvu hata za kusimama,atakuwa kazidiwa nguvu,kapita anga
mbaya”,Hamis Mayunga aliiambia Malunde1 blog.
Naye mjumbe wa serikali ya mtaa wa Mageuzi
Waziri Mussa(Chadema) alikiri kuwepo kwa tukio hilo ambalo lilijaza umati wa
watu, huku wakishindwa kumtambua kikongwe huyo wapi alikuwa akitoka wala
anapokwenda kutokana na maswali waliyokuwa wakimuuliza na kushindwa kuongea
maneno sahihi zaidi ya yale ya ushirikina.
Hata hivyo Mussa alisema, wakati wakiendelea
kumuhoji ndipo bibi huyo alipozidi kupata fahamu ambapo pia walimpatia uji ili
kupata nguvu, lakini kutokana na kutomtambua na kushindwa kuelewana ili bidi
aongee na wanazengo akawasihi wasimdhuru na kuita jeshi la polisi.
Jeshi la polisi lilifika eneo la tukio na
kumkuta bibi huyo tayari ameanza kupata nguvu kisha kuwaomba wakazi wa eneo
hilo wamuache kikongwe huyo aendelee na safari zake kutokana na kwamba serikali
haimini uchawi.