WANAFUNZI WASAHIHISHA MITIHANI YA WANAFUNZI WENZAO- SHINYANGA




Imeelezwa kuwa walimu katika shule ya msingi Mwenge iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga wanatumia wanafunzi wao kusahihisha mitihani ya  wanafunzi wenzao hali ambayo imetajwa kuchangia kushuka kwa kiwango cha elimu katika shule hiyo.

 Wakizunguza katika kikao cha wazazi na walezi wa wanafunzi kilichoenda sambamba na  kufunga shule hiyo kilichofanyika katika shule hiyo mjini Shinyanga wazazi na walezi hao wameeleza kukerwa na tabia iliyoanzishwa na walimu kutumia wanafunzi kusahihisha mitihani ya wanafunzi wenzao hali inayohatarisha ufaulu wa wanafunzi hao kwani hakuna umakini wowote katika usahihishaji huo ambapo penye kosa huwekwa vema.

Akizungumzia kuhusu suala hilo mgeni rasmi , ambaye ni Katibu tawala wa wilaya ya Shinyanga bwana Boniface Chambi alisema walimu katika shule ya msingi Mwenge hawafanyi maksudi bali tatizo hilo linatokana na idadi ndogo ya walimu ukilinganisha na idadi ya walimu waliopo shuleni hapo.

Amesema Katika shule hii kuna walimu 21 pekee wakati wanafunzi wako 1200,hivyo walimu wanalazimika kutumia wanafunzi wenye uwezo mkubwa darasani wa madarasa ya juu ili kuwasaidia wadogo zao

Naye mwalimu mkuu wa shule hiyo bwana Mahamudu Ibrahim amesema suala hilo linajitokeza zaidi wakati wa mitihani kwa ajili ya kuandaa haraka matokeo pindi shule inapofungwa tatizo linalochangiwa na uhaba wa walimu shuleni hapo.

 Hata hivyo mwalimu huyo mkuu amesema ili kuhakikisha matokeo kwa wanafunzi wake yanakuwa mazuri,walimu katika shule hiyo wanalazimika kufundisha kuanzia asubuhi hadi saa 12 jioni badala ya kuishia saa 8 :30 mchana kama inavyotakiwa.

Kwa upande wao wazazi na walezi wa wanafunzi waliohudhuria kikao hicho wameiomba serikali kuiangalia kwa jicho la huruma shule hiyo kwa kuongeza walimu wa kutosha kwani ni aibu kubwa sana kwa wanafunzi kusahihisha mitihani ya wanafunzi wenzao na kitendo hicho inapelekea kushuka kwa kiwango cha elimu hapa nchini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم