Imeelezwa kuwa wanawake wengi katika wilaya ya
kishapu iliyopo mkoani shinyanga wanakabiliwa changamoto ya kuvunja ndoa zao
kutokana na umbali uliopo ili kupata huduma ya maji,ambapo hulazimika kuamka
kila siku saa 11 alfajiri kufuata hduma ya maji kwa takribani kilomita kumi na tayari ndoa zaidi ya kumi zimevunjika kwa sababu hiyo.
Hayo yamebaishwa leo na wananchi wa wilaya hiyo katika warsha ya siku tatu inayoendelea, kwa waandishi
wa habari kuhusu harakati za mwanamke na mchakato wa katiba mpya iliyoandaliwa
na Mtandao wa jinsia Tanzania TGNP katika viwanja vya Mazingira Senta mjini
Shinyanga.
Mmoja wa washiriki katika warsha hiyo Bi Sesilia
John,kutoka Kikundi cha Nyuki cha Kishapu ambacho kiko chini ya TGNP
amesema wanawake wengi wa Kishapu wanavunja
miji yao kutokana na adha ya maji ambapo
hulazimika kuwaacha wanaumme wao kila siku saa 11 alfajiri hali inayosababisha wanaumme hao kuwa na
uhusiano wa kimapenzi na wanawake wengine,matokeo yake ndoa zinavunjika.
“Wanawake wa kishapu pia wanabakwa,kupigwa na hata
kuvamiwa na wanyama aina ya fisi pindi wanapofuata huduma ya maji nyakati za
usiku,mfano katika kijiji cha Lubaga na Isoso,na ukosegu huu wa maji pia
unasababisha hata kufa kwa mifugo yetu”,Bi Sesilia amesema.
Naye
mwenyekiti wa Kikundi hicho cha Nyuki Bi Anna Christopher amesema licha ya
kuwepo kwa tatizo la maji pia shule nyingi za sekondari wilayani humo hazina
walimu wa kutosha,michango katika shule pia ni mingi sana, na jambo la
kushangaza shule ya sekondari Isoso
iliyojengwa mwaka 2006 haina hata mwanafunzi mmoja.
Katika hatua nyingine Afisa wa Habari na mawasiliano
wa TGNP,Bi Scholastica Makwaia,amesema hivi karibuni mtandao wa jinsia Tanzania
ulifanya ziara ya wiki tatu wilayani humo na kubaini kuwa bado kuna ukatili kwa
wanawake,na aliainisha aina mbili za ukatili huo yaani ukatili wa kimwili na
ule wa kiuchumi ambapo mwanamke hutumia muda mwingi kulima na wakati wa mavuno
wanaumme ndio wanakuwa wauzaji wakuu wa mazao yaliyopatikana.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Idara ya Habari na
Mawasiliano kutoka TGNP Bi Lilian Liundi ametaja miongoni mwa malengo
ya warsha hiyo kuwa ni kuendelea kujenga uelewa kwa wanahabari kuhusu harakati za
ukombozi wa wanawake kwenye mchakato wa uundwaji wa katiba mpya.
Amefafanua pia kuwa warsha hiyo ni kutafakati kwa
pamoja miaka 20 ya harakati za wanawake
TGNP ambayo ilianzishwa mwaka 1993,pamoja na tamasha la jinsia mwaka 2013,
sambambamba na kujadili mikakati ya baadae katika kupashana habari kuhusu mambo
ya jinsia katika jamii.