Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limetangaza kuanza kwa usaili wa vijana wanaotarajia kujiunga na mafunzo ya kujitolea kwa mwaka 2026/27, huku likitoa kipaumbele kwa waombaji wenye taaluma mbalimbali za ufundi na teknolojia ya habari na mawasiliano.
Wito huo umetolewa leo, Novemba 12, 2026, jijini Dodoma na Mkuu wa Tawi la Utawala wa JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena, kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Nduka Mabele, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Jeshi hilo.
Amesema usaili wa vijana hao utaanza Novemba 16, mwaka huu, katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani na kwamba vijana watakaofaulu usaili na kuchaguliwa kujiunga na mafunzo hayo wanatakiwa kuripoti katika makambi ya JKT kuanzia Desemba 10 hadi 15, 2026.
"Utaratibu wa kuomba nafasi hizo na kuchaguliwa kwa waombaji unasimamiwa na Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanakoishi vijana husika,"ameeleza
Katika wito huo, JKT limewahimiza vijana wenye taaluma za teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kujitokeza kuomba nafasi hizo, wakiwemo wenye stashahada na shahada katika fani za Sayansi ya Kompyuta, Teknolojia ya Habari, Uhandisi wa Kompyuta, Mifumo ya Taarifa za Biashara, Usalama wa Mtandao na Uchunguzi wa Kitaalamu wa Uhalifu wa Kidijitali.
"Vijana wanaohitajika ni wenye ujuzi wa ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (VET), katika fani za uchomeleaji, ufundi magari, umeme wa magari, ufundi bomba, upakaji rangi, uashi, ubunifu wa mavazi, ukarani, useremala, ushonaji pamoja na ufundi wa friji na viyoyozi,"amefafanua
Ameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kupata vijana wenye taaluma na ujuzi mbalimbali watakaoweza kunufaika na mafunzo ya JKT yanayojumuisha stadi za kazi na maisha, pamoja na kujengewa uzalendo, umoja wa kitaifa na ukakamavu.
Hata hivyo, ameweka wazi kuwa nafasi hizo za mafunzo hazipaswi kuchukuliwa kama njia ya moja kwa moja ya kupata ajira Serikalini au katika taasisi nyingine.
Amesisitiza kuwa Jeshi hilo halitoi ajira wala halihusiki kuwatafutia wahitimu ajira katika asasi, vyombo vya ulinzi na usalama, mashirika ya serikali au yasiyo ya kiserikali.
Badala yake, mafunzo hayo yanalenga kuwajengea vijana uwezo na stadi zitakazowawezesha kujiajiri baada ya kumaliza mikataba yao na Jeshi hilo.
"Tunawaomba vijana wanaotaka kuomba nafasi hizo kusoma sifa za waombaji na maelekezo ya vifaa wanavyopaswa kwenda navyo kupitia tovuti rasmi ya Jeshi hilo ambayo ni www.jkt.mil.tz."amesema
Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Mabele, amewakaribisha vijana watakaopata nafasi hiyo kujiunga na wenzao ili kupata mafunzo yatakayowajenga katika uzalendo, umoja wa kitaifa, ukakamavu na utayari wa kulijenga na kulitumikia Taifa.

TAFUTA HABARI
Social Plugin