Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DRC YAVUTIWA NA MAENDELEO YA MIUNDOMBINU, MJI WA SERIKALI MTUMBA





Na Dotto Kwilasa,Dodoma

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Judith Suminwa Tuluka, ameonesha kuvutiwa na hatua za maendeleo ya miundombinu zilizofikiwa na Tanzania, hususan uwekezaji katika majengo ya umma na ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, akieleza kuwa hatua hizo ni mfano wa uwekezaji unaoweza kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Kutembelea kwake Mji wa Serikali Mtumba kumempa fursa ya kujionea uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha miundombinu ya kiutawala na kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za umma.

Ziara hiyo pia imefungua fursa ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na DRC katika sekta mbalimbali, zikiwamo miundombinu, uchumi na usalama.

Akizungumza leo November 4,2026 wakati wa ziara hiyo Dodoma ,Waziri Mkuu huyo ameishukuru Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kushirikiana na DRC katika masuala ya usalama na maendeleo ya kiuchumi, akisema ushirikiano huo una umuhimu mkubwa katika kulinda maslahi ya mataifa hayo mawili.

Amesema Tanzania na DRC zina uhusiano wa muda mrefu uliojengwa katika misingi ya undugu na ujirani mwema, hivyo ni muhimu kuendeleza ushirikiano huo kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi wa DRC, John Banza Lunda, amesema amevutiwa na maendeleo ya miundombinu aliyoyashuhudia nchini Tanzania, akieleza kuwa safari yake kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma imempa nafasi ya kujionea uwekezaji katika sekta ya usafiri na majengo ya umma.

Ametaja miundombinu ya Bunge na Mji wa Serikali Mtumba kuwa miongoni mwa miradi iliyomvutia, akisema Tanzania imepiga hatua katika kujenga miundombinu inayorahisisha utoaji wa huduma na kuchochea shughuli za kiuchumi.

Amesema DRC nayo inaendelea kuweka juhudi katika kujenga na kuboresha miundombinu ili kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Aidha, amesema anatarajia kutumia Treni ya Reli ya Kisasa (SGR) kurejea Dar es Salaam ili kujionea zaidi uwekezaji wa Tanzania katika sekta ya usafiri wa reli.

Katika hatua nyingine, Banza Lunda amesema DRC inaendelea na juhudi za kuendeleza bandari katika mwambao wa Ziwa Tanganyika, inayotarajiwa kuanza kufanya kazi Machi 2027.

Amesema bandari hiyo itakuwa kichocheo muhimu cha kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kukuza biashara katika maeneo yanayozunguka Ziwa Tanganyika, pamoja na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.

Naye Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, amesema Tanzania imefurahi kupokea ujumbe wa DRC kwa ziara ya kindugu na kirafiki inayolenga kuimarisha uhusiano wa muda mrefu kati ya mataifa hayo.

Kairuki amesema uhusiano wa Tanzania na DRC umejengwa kwa muda mrefu katika misingi ya historia ya pamoja, undugu na ujirani mwema, akieleza kuwa ziara hiyo ni fursa ya kuendeleza mshikamano na kufungua milango ya ushirikiano katika sekta mbalimbali.

Ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kuthamini uhusiano huo na kujenga mazingira mazuri ya ushirikiano kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo mbili.









Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com