Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TRA UNITED FC YAZINDUA WIKI MAALUM, YAALIKA WANANCHI KUJITOKEZA KWA WINGI



Na Bora Mustafa, Arusha.

Timu ya TRA United FC imezindua wiki maalum ya shughuli mbalimbali kuelekea mchezo wake wa kwanza wa nyumbani katika Ligi Kuu ya NBC, huku uongozi wa timu hiyo ukiwaalika wananchi wa Arusha na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kuipa sapoti.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Jumamosi, Agosti 29, katika Uwanja wa Machinjio, ambapo TRA United FC itakutana na Dodoma jiji, katika mchezo ambao utakuwa wa kwanza kwa timu hiyo kucheza nyumbani Arusha katika msimu huu.

Akizungumza Leo Agosti 26,2026 katika mkutano na waandishi wa habari, Manager wa TRA United FC, Deogratius Shuma, amesema kurejea kwa timu hiyo Arusha ni jambo la muhimu, huku akieleza kuwa tayari imeanza kuonesha kiwango kizuri katika michezo iliyopita.

Shuma amesema katika michezo dhidi ya Tanzania Prisons, Azam FC na Coastal Union, timu imeonesha soka la ushindani na uwezo wa kupambana bila kujali kama mchezo umechezwa nyumbani au ugenini.

Amesema mwenendo huo unaonesha mabadiliko yaliyofanyika ndani ya timu na kwamba mashabiki watapata nafasi ya kushuhudia kwa macho yao kiwango ambacho TRA United FC imefikia.

“Timu ilikuwa inacheza mchezo mzuri, inacheza mchezo wa ushindani bila kujali kwamba iko nyumbani au iko ugenini,” amesema Shuma.

Aidha, Shuma amewashukuru wadau wa michezo na wananchi wa Mkoa wa Arusha kwa namna walivyoipokea TRA United FC na kuichukulia kama sehemu ya timu zao, pamoja na kujitokeza katika michezo iliyopita kuipa sapoti.

Amesema uwepo wa mashabiki kwa wingi ni muhimu katika kuongeza morali kwa wachezaji na kuipa timu nguvu ya kupambana kupata matokeo mazuri.

Kwa upande wake, Afisa Habari wa TRA United FC, Christina Mwagala, amesema timu imeandaa wiki maalum yenye shughuli mbalimbali kuelekea mchezo huo wa kwanza wa nyumbani.

Mwagala amesema timu inalenga pia kutumia vyombo vya habari kufikisha taarifa za TRA United FC kwa wananchi wa Arusha na kuwaandaa kwa mchezo huo.

Amesema shughuli hizo zitaanza kabla ya siku ya mchezo na zitahusisha matukio mbalimbali, ikiwemo shughuli za kurejesha Fadhila kwa jamii.

Aidha, amesema TRA United FC imepanga kutembelea baadhi ya vituo na maeneo yanayohudumia watoto jijini Arusha, pamoja na kuwafikia watoto yatima kama sehemu ya kuendelea kuwa karibu na jamii.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya timu kuhakikisha inatumia nafasi yake siyo tu kushiriki mashindano, bali pia kutoa mchango chanya kwa jamii inayowazunguka

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com