Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JINA LA NDEJEMBI LAVURUGA UBASHIRI WA WENGI



Na Dotto Kwilasa,DODOMA, Agosti 26, 2026

Mjadala kuhusu atakayemrithi Dkt. Emmanuel Nchimbi katika nafasi ya Makamu wa Rais umechukua sura mpya baada ya jina la Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, kuibuka kama chaguo lililopendekezwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ndejembi ameibuka siku moja tu baada ya Nchimbi kutangaza kujiuzulu nafasi hiyo, akieleza kuwa uamuzi wake utaanza kutekelezwa Septemba 4, 2026, huku pia akitangaza kustaafu siasa na utumishi wa umma.

Kujiuzulu kwa Nchimbi kulifungua mjadala mpana nchini kuhusu nani angepewa nafasi ya kuendeleza majukumu ya Makamu wa Rais.

Katika mijadala hiyo, majina kadhaa yalitajwa na kubashiriwa, lakini Ndejembi hakuwa miongoni mwa waliokuwa wakitajwa zaidi.

Hata hivyo, hali imebadilika baada ya Halmashauri Kuu ya CCM, chini ya Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, kumpendekeza Ndejembi kwa nafasi hiyo.

Uteuzi huo unaifanya safari ya kisiasa ya Ndejembi kuingia katika hatua nyingine kubwa.

Kabla ya jina lake kuibuka katika nafasi ya Makamu wa Rais, alikuwa akiongoza Wizara ya Nishati, nafasi aliyokabidhiwa baada ya kuapishwa na Rais Samia katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, Novemba 2025.

Akiwa Waziri wa Nishati, Ndejembi amekuwa akihusika na usimamizi wa masuala muhimu katika sekta hiyo, ikiwamo uzalishaji na usafirishaji wa umeme, upatikanaji wa mafuta pamoja na uendelezaji wa miundombinu ya nishati nchini.

Kwa namna ya pekee, kuibuka kwake sasa kunatoa taswira ya mabadiliko ya haraka katika safu ya uongozi wa Serikali, kwani ndani ya kipindi kifupi ametoka kuongoza wizara nyeti na sasa anatajwa kwa nafasi ya pili kwa ukubwa katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hatua hiyo imekuja baada ya Nchimbi kuhitimisha safari yake katika nafasi ya Makamu wa Rais, akisema amefanya uamuzi huo baada ya kutafakari kwa kina na kwamba ataendelea kulitumikia Taifa kama raia mwema hata baada ya kustaafu siasa na utumishi wa umma.

Kwa sasa, macho yanaelekezwa kwenye hatua zinazofuata za mchakato wa kikatiba na uteuzi.

Jina la Ndejembi, ambalo halikutawala katika orodha za awali za waliokuwa wakibashiriwa, sasa limegeuka kuwa moja ya majina muhimu zaidi katika mjadala wa kisiasa nchini.

Hatua hii imetoa funzo kuwa Wakati mwingine Mungu hufanya jambo kwa namna ambayo hakuna anayetarajia.

Kwa wanaoamini itoshe tu kusema  “Mungu huinua mtu kwa wakati wake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com