
Wakurugenzi Wanawake wa mashirika yasiyo ya kiserikali Tanzania wameazimia kuongeza nguvu za kutetea mabadiliko ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ili kuwaepusha Watoto wa kike na ndoa za utotoni.
Maazimio hayo yalitolewa hivi karibuni kwenye jukwaa la wakurugenzi hao lililoandaliwa na WiLDAF kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ikiwemo uzinduzi wa awamu ya tatu ya huduma za ukungwi (mentorship program).
Maazimio mengine ni pamoja na kuboresha huduma za afya ya akili kwa Watoto na kuongeza watalamu pamoja na kuwalinda dhidi ya adhabu ya viboko.
Sheria ya Ndoa inapingana na Sheria zingine ambazo zinafafanua tafsiri ya mtoto. Wakati Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, inamwelezea mtoto kama mtu mwenye umri chini ya miaka 18, Sheria ya Ndoa bado inamruhusu mtoto mwenye umri wa miaka 15 kuolewa kwa ruhusa ya wazazi.
Mwaka 2019, Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ilithibitisha uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi ya Rebeca Gyumi dhidi ya MwanaSheria mkuu wa Serikali, kuwa vifungu vya 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa ambavyo vinaruhusu mtoto kuolewa na umri wa miaka 15 kwa idhini ya wazazi na 14 kwa ruhusa ya mahakama ni vya kibaguzi dhidi ya mtoto wa kike na ni kinyume na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo utekelezaji wa maamuzi hayo bado haujafanyika jambo ambalo limeendelea kuwaweka Watoto wa kike katika hatari ya kuozwa katika umri mdogo.
Ndoa za utotoni, zinazofafanuliwa kama ndoa inayohusisha mmoja au wote wawili walio chini ya umri wa miaka 18, bado ni tatizo kubwa nchini Tanzania licha ya juhudi za kimataifa na kitaifa za kukomesha vitendo hivyo.
Tatizo hili linaathiri zaidi watoto wa kike, ambao mara nyingi hulazimishwa kuingia kwenye ndoa wakiwa na umri mdogo, hali inayowanyima haki yao ya msingi ya kukua, kupata elimu, kuathiri afya zao, na kuwaweka katika hatari kubwa ya unyanyasaji wa kijinsia, kifamilia na kiuchumi.
TKwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi na Haki za Kijinsia (UNFPA-Tanzania) ndoa za utotoni zimechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa idadi ya wasichana wanaokatisha masomo, hususani katika maeneo ya vijijini.
Katika maeneo mengi ya pembezoni, mila na desturi pamoja na umaskini husababisha wazazi kuwaona watoto wa kike kama mzigo wa kiuchumi, hivyo kuwalazimisha kuolewa mapema badala ya kuendelea na elimu, linasema shirika hilo.
Malengo ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu UN (SDGs; 2015) Lengo la 5.3 linazielekeza nchi zote wanachama kumaliza kabisa tatizo la ndoa za utotoni ifikapo mwaka 2030.
Azimio la Kutokomeza Aina zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW; 1979) linazitaka serikali zichukue hatua madhubuti kuhakikisha kwamba “kuposwa na kuolewa kwa mtoto hakutakubalika kisheria
Social Plugin