NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Hatua ya Benki ya Biashara ya Mwalimu (MCB) kuuza hisa stahiki imeelezwa kuwa chachu ya kuimarisha mtaji na kupanua wigo wa utoaji wa mikopo nafuu kwa walimu pamoja na wafanyabiashara wadogo nchini.
Hayo yameelezwa leo Mei 6, 2026 Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mpango wa uuzaji wa hisa stahiki wa Benki ya Biashara ya Mwalimu ikilenga kuongeza mtaji wa benki, kuongeza uwekezaji na kuimarisha utoaji wa mikopo nafuu kwa walimu na wafanyabiashara wadogo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Waziri Mkuu Mstaafu, Kassimu Majaliwa, amesema uuzaji wa hisa stahiki unatoa fursa kwa wanahisa kuongeza umiliki wao huku benki ikiimarisha uwezo wake wa kifedha.
Amesema kupitia mpango huo, MCB itaongeza mtaji, kupanua huduma kwa wananchi wengi zaidi, kuimarisha utoaji wa mikopo nafuu kwa walimu, wafanyakazi na wafanyabiashara wa kati na wadogo, pamoja na kuendeleza teknolojia za kidigitali.
“Si fursa ya kifedha pekee, bali ni nafasi ya kuchangia ukuaji wa benki na maendeleo ya uchumi wa taifa,” amesema Majaliwa, akiwahimiza wanahisa kushiriki kikamilifu katika ununuzi wa hisa hizo.
Mpango huo unasimamiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), huku utekelezaji wake ukiongozwa na iTrust Finance Limited.
Mwenyekiti wa Bodi ya MCB, Francis Ramadhani, amesema wanahisa wote waliokuwa kwenye rejesta kufikia Mei 5, 2026 wanastahili kununua hisa mpya tatu kwa kila hisa moja waliyonayo, kwa bei ya punguzo ya Sh 110.
Ameongeza kuwa dirisha la ununuzi limefunguliwa, ambapo wanahisa wanaweza kununua hisa hizo kidigitali kupitia DSE Hisa Kiganjani, ofisi za Chama cha Walimu (CWT), pamoja na matawi ya benki hiyo.
Ramadhani amesema mpango huo umepata idhini ya Benki Kuu (BOT) na unatekelezwa kwa uwazi chini ya usimamizi wa CMSA na DSE, akisisitiza umuhimu wa wanahisa kushiriki ili kuimarisha mtaji wa benki na kukidhi matakwa ya kisheria.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa MCB, Richard Makungwa, amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita benki hiyo imeonyesha ukuaji mkubwa wa kifedha.
Alisema mali za benki zimeongezeka kutoka chini ya Sh bilioni 30 mwaka 2019 hadi Sh bilioni 98 mwaka 2025, huku amana za wateja zikikua kutoka Sh bilioni 16 hadi zaidi ya Sh bilioni 75 katika kipindi hicho.
Aidha, mikopo imeongezeka kutoka Sh bilioni 16 hadi Sh bilioni 66, ikilenga zaidi walimu na wafanyabiashara wadogo na wa kati, huku faida kabla ya kodi ikibadilika kutoka hasara ya Sh bilioni 4.8 mwaka 2019 hadi faida ya Sh milioni 487 mwaka 2025.
Ukuaji huo, amesema, unaakisi ufanisi wa usimamizi wa rasilimali, kuongezeka kwa imani ya wateja na mwelekeo chanya wa biashara wa benki hiyo.
Waziri Mkuu Mstaafu, Kassimu Majaliwa (katikati) akipiga makofi baada ya kuzindua mpango wa uuzaji wa hisa stahiki wa Benki ya Biashara ya Mwalimu ikilenga kuongeza mtaji wa benki, kuongeza uwekezaji na kuimarisha utoaji wa mikopo nafuu kwa walimu na wafanyabiashara wadogo. Hafla hiyo imefanyika leo Mei 6, 2026 Jijini Dar es Salaam
Waziri Mkuu Mstaafu, Kassimu Majaliwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango wa uuzaji wa hisa stahiki wa Benki ya Biashara ya Mwalimu ikilenga kuongeza mtaji wa benki, kuongeza uwekezaji na kuimarisha utoaji wa mikopo nafuu kwa walimu na wafanyabiashara wadogo. Hafla hiyo imefanyika leo Mei 6, 2026 Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya MCB, Francis Ramadhani akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango wa uuzaji wa hisa stahiki wa Benki ya Biashara ya Mwalimu ikilenga kuongeza mtaji wa benki, kuongeza uwekezaji na kuimarisha utoaji wa mikopo nafuu kwa walimu na wafanyabiashara wadogo. Hafla hiyo imefanyika leo Mei 6, 2026 Jijini Dar es Salaam.
















Social Plugin