
Serikali kupitia Wizara ya Afya imetangaza rasmi washindi wa mashindano ya usafi wa mazingira kwa mwaka 2026, yakihusisha ngazi zote kuanzia majiji, manispaa, miji, wilaya hadi mitaa, vijiji, shule na taasisi mbalimbali, jambo linaloonesha mwamko mkubwa wa jamii katika kulinda afya kupitia mazingira safi.
Tuzo hizo zilitolewa na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Afya Kitaifa yaliyofanyika Wilayani Kibiti, Mkoani Pwani.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Mchengerwa alisisitiza kuwa usafi wa mazingira ni silaha muhimu katika kuzuia magonjwa na kuboresha ustawi wa wananchi.
Katika kundi la majiji, Jiji la Arusha liliibuka mshindi wa kwanza, likifuatiwa na Jiji la Mwanza na Jiji la Tanga.
Kwa upande wa manispaa, Manispaa ya Shinyanga iliongoza kupitia Mtaa wa Miti Mirefu unaoongozwa na Mwenyekiti Nassor Warioba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Mitaa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, ikifuatiwa na Manispaa ya Iringa na Manispaa ya Moshi.
Kwa halmashauri za miji, Mji wa Njombe ulishika nafasi ya kwanza, ukifuatiwa na Mji wa Mafinga na Mji wa Babati. Katika halmashauri za wilaya, Wilaya ya Njombe iliongoza, ikifuatiwa na Wilaya ya Makete na Wilaya ya Mufindi.
Ngazi ya mitaa ilionesha ushindani mkubwa ambapo Mtaa wa Kwivaba uliopo Mji wa Njombe uliibuka mshindi wa kwanza, ukifuatiwa na Mtaa wa Mereni uliopo Manispaa ya Moshi, huku nafasi ya tatu ikienda kwa Mtaa wa Miti Mirefu uliopo Manispaa ya Shinyanga.
Kwa upande wa vijiji, Kijiji cha Ihanga’na kilichopo Wilaya ya Njombe kilishika nafasi ya kwanza, kikifuatiwa na Kijiji cha Ukalawa kilichopo Wilaya ya Njombe, na nafasi ya tatu kuchukuliwa na Kijiji cha Utanziwa kilichopo Wilaya ya Makete.
Katika shule za msingi za Serikali, Shule ya Msingi Ihanga’na iliyopo Wilaya ya Njombe iliibuka mshindi wa kwanza, ikifuatiwa na Shule ya Msingi Ukalawa iliyopo Wilaya ya Njombe, huku nafasi ya tatu ikienda kwa Shule ya Msingi Azimio iliyopo Jijini Mbeya.
Kwa upande wa shule za sekondari za bweni, Shule ya Sekondari Ahmes Mbweni iliyopo Mkoa wa Dar es Salaam iliongoza, ikifuatiwa na Shule ya Sekondari Nyango iliyopo Wilaya ya Mtama Mkoani Lindi, na nafasi ya tatu kuchukuliwa na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya St. Francis iliyopo Mbeya.
Katika sekta ya afya, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha (Mount Meru) iliibuka mshindi wa kwanza, ikifuatiwa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, huku nafasi ya tatu ikienda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana. Kwa hospitali za halmashauri, Hospitali ya Mji wa Njombe iliongoza, ikifuatiwa na Hospitali ya Wilaya ya Chunya na nafasi ya tatu kuchukuliwa na Hospitali ya Mji wa Mafinga.
Katika vyuo vikuu, Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) iliibuka mshindi wa kwanza, ikifuatiwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, huku Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) kikishika nafasi ya tatu.
Mhe. Mchengerwa alieleza kuwa mashindano hayo yamekuwa chachu ya kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira yao, akisisitiza kuwa mazingira safi ni msingi wa afya bora na maendeleo endelevu.
Maadhimisho ya Wiki ya Afya Kitaifa yamekuwa jukwaa muhimu la kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu kinga dhidi ya magonjwa, usafi wa mazingira na umuhimu wa kushirikiana katika kujenga taifa lenye afya njema.






















































Social Plugin